Habari Mseto

Prof Ojienda aendelee kuchunguzwa – Mahakama

February 10th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Juu imefutilia mbali agizo lililoizima tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) kuchunguza akaunti za wakili mwenye tajriba ya juu Prof Tom Ojienda.

Jaji Mkuu David Maraga, Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala na Noki Ndung’u walisitisha agizo la kuzuia EACC kuchunguza akaunti za Prof Ojienda hadi rufaa iliyowasilishwa isikizwe na kuamuliwa.

Mahakama ya rufaa ilikuwa imetoa agizo la kusitisha agizo la Mahakama kuu iliyokuwa imefikia uamuzi haki za Prof Ojienda zilikuwa zimekandamizwa akaunti zake zilipochunguzwa bila idhini yake.

EACC ilikuwa imepata kibali kutoka kwa Mahakama ya Kibera kuchunguza akaunti za benki za wakili huyo kwa madai alikuwa amepokea malipo ya Sh280m kutoka kwa kampuni ya Sukari ya Mumias (MSC).

Mahakama kuu ilisema katika uamuzi huo kuwa EACC ilikandamiza haki za Prof Ojienda kwa kuruhusu wapelelezi kumulika akaunti zake bila ya kumwarifu.

Jaji Maraga na wenzake wanne walisema vita dhidi ya ufisadi ni suala lililo na umuhimu mkuu kwa umma.

“Ikitiliwa maanani suala hili linaathiri msalaha ya umma ni wazi mwongozo wahitajika kutoka mahakama hii ya upeo,” walisema majaji hao watano wakiongozwa na rais wa mahakama hiyo Jaji Maraga.

EACC ilikuwa imeeleza mahakama kuwa agizo la kutolewa kwa arifa ya kuchunguza akaunti za washukiwa liko na athari tele “ katika vita vya kupambana na ufisadi.”.

EACC inadai inahitaji uchunguzi wa kina ndipo mahojiano inayoendeleza yapate ufanisi.

EACC inasema kuwa maombi mengi yamewasilishwa katika mahakama tofauti tofauti kuhusu kufichiluwa na kuchunguwa kwazo.

EACC imesema maagizo yametolewa na mahakama mbali mbali za kuachiliwa kwa hati zilizotwaliwa nalo.

Kesi hii ilianza Machi18, 2015, wakati mahakama ya Kibera ilipoikubalia EACC kuchunguza akaunti zake za benki.

Agizo la kuchunguzwa kwa akaunti hizo za Prof Ojienda lilitokana na madai wakili huyo alipokea kitita cha Sh280m kutoka kwa kiwanda hicho cha MSC kinachokumbwa na matatizo ya kifedha.