Makala

PROLACTINOMA: Ugonjwa wa kutoa maziwa kwa matiti unaomhangaisha pasta wa jijini

May 29th, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MHUBIRI mmoja jijini Nairobi amejitokeza kimasomaso kusema kuwa hajafurahia burudani kitandani na mkewe kwa zaidi ya miaka kumi kutokana na tatizo la kiafya la aina yake.

Pasta Francis Gichuru Gachieki, mhubiri na mwasisi wa kanisa la Christ Ambassadors Church International lililoko katika eneo la Mowlem, Nairobi, hajafurahia tendo la ndoa tangu 2009, baada ya kuugua prolactinoma, ugonjwa unaosababisha matiti yake kutoa maziwa.

Pasta huyo anasema hamu yake ya ngono imeisha, lakini hajatamauka kuchangisha fedha kufanyiwa upasuaji kumrudisha kwa raha ya maisha ya ndoa.

Ugonjwa huo husababisha ukosefu wa hamu ya uroda, kupungua kwa madini ya Calcium, kuvurugika kwa homini na hata utasa.

“Tatizo hili lilianza pindi tu tulipofanya harusi mwaka 2000, singeweza kumridhisha mke wangu, lakini hatungejua kiini,” anasema.

Gichuru anasema kuwa licha ya ugonjwa huu, bado baadhi ya marafiki na watu wa familia humsuta kwa kukosa kupata mtoto.

“Baada ya kutoka kwa saibakafe mnamo 2007, niligundua kuwa nilikuwa na majimaji yasiyoeleweka kwa shati langu, lakini nikapuuza.

“Zaidi ya madaktari watatu wamenifanyia uchunguzi. Kwa wakati mmoja, kundi loa madaktari na wanafunzi lilinitoa nguo zote huku wakiduwaa.”

Msaada ulijiri 2007 wakati alipokuwa akisikiza redio ambao alisikia daktari wa kike akielezea kuhusu ugonjwa huo na kusema kuwa ulikuwa na tiba.

Alipokutana na daktari huyo, alipewa tembe za dawa ambazo angalau zilimtuliza akili.

“Lakini ugonjwa huu uliponilemea 2014, daktari wangu alinishauri nisafiri India, Amerika, Singapore au Israeli kwa upasuaji. Upasuaji huu utakuw amuhimu sana kwangu kwa kuwa umenipotezea hamu ya maisha, anasema.

Pasta huyu anasema kwa sasa anajisi mnyonge na ameongeza uzani kupindukia na hawezi kufurahia baadhi ya mapochopocho ya vyakula.

Kufikia sasa ametumia Sh1.3 milioni kwa kwa matibabu lakini madaktari wamesema anahitajizaidi ya Sh2.5 milioni kufanyiwa upasuaji kikamilifu.

Kutokana na hali hii ya kiafya, kanisa lake limepata pigo kuu, huku baadhi ya waumini wakihamia makanisa mengine wakidai “hatuwezi kuongozwa na mwanamume asiye na watoto.”