Habari

PSC kupambana na Maraga kortini

September 22nd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

TUME ya Huduma za Bunge (PSC) itawasilisha kesi katika mahakama kuu kupinga hatua ya Jaji Mkuu David Maraga kumshauri Rais Uhuru Kenyattta kuvunja bunge.

Mwenyekiti wa tume hiyo Justin Muturi ambaye pia ndiye Spika wa Bunge la Kitaifa, Jumanne aliutaja kama uamuzi ambao ulitolewa kwa pupa kinyume cha Katiba.

“Tume inasikitika Jaji Mkuu anaonekana yuko tayari kulitumbukiza taifa hili katika lindi la mzozo wa kikatiba bila kutumia hekima anayotakikana kuwa nayo akiwa ndiye aliye katika afisi kuu kama hiyo,” Bw Muturi akasema.

Spika huyu alisema bunge halifai kulaumiwa kwa suala hilo, kwa sababu kipengele za 27 (7) cha Katiba kinasema kuwa wajibu wa kupitishwa na sheria hiyo ni wa serikali kwa ujumla.

“Serikali inayorejelewa kwenye Katiba ina matawi matatu; Afisi Kuu, Bunge na Idara ya Mahakama. Kwa hivyo, isiwe kwamba ni bunge pekee ndilo linalaumiwa kwa kutopitishwa kwa sheria hii?” akaeleza Bw Muturi.

Kwa misingi hii, PSC imeagiza mawakili wake waende mahakamani kupinga agizo hilo la Bw Maraga.

“Jaji Mkuu alitoa ushauri wake bila kuzingatia kuwa kuna kesi mbili zinazopinga agizo lililotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu John Mativo mnamo Machi 29, 2017. Kesi hiyo inalenga kubaini ikiwa agizo hilo lililotolewa wakati wa muhula wa bunge la 11 linaweza kuzingatiwa na bunge la 12, akasema Bw Muturi ambaye alikuwa ameandamana na wanachama wengine wa PSC.

Katika barua aliyomwandikia Rais Kenyatta Jumatatu, Jaji Mkuu anamshauru kuvunja bunge kutokana na maombi sita aliyopokea kutoka kwa wanaharakati kadhaa pamoja na Chama cha Mawakili Nchini (LSK).

Hii ni baada ya watu hao na LSK kulilaumu Bunge kwa kufeli sheria ya kuhakikisha uwepo wa usawa wa kijinsia katika asasi zote za umma.