Michezo

PSG kupumua baada ya waratibu kusogeza tarehe ya kuanza kwa Ligue 1

August 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

PARIS Saint-Germain (PSG) watakuwa na siku 12 zaidi za kujiandaa kwa msimu mpya wa 2020-21 katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) baada ya vinara wa soka ya Ufaransa kukubali kuratibu upya mechi zao.

PSG walitazamiwa kupepetana na Lens katika mchuano wao wa ufunguzi wa msimu huu mnamo Agosti 29, 2020, zikiwa ni siku sita baada ya kupigwa 1-0 na Bayern Munich kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Hata hivyo, mechi hiyo kwa sasa itasakatwa Alhamisi ya Septemba 12, 2020, baada ya likizo ya michuano ya kimataifa.

Kampeni mpya za Ligue 1 kwa minajili ya msimu huu zilianza wikendi iliyopita ya Agosti 22 bila PSG waliokuwa wakijiandaa kwa gozi dhidi ya Bayern kushirikishwa.

PSG walitawazwa mabingwa wa Ligue 1 msimu huu kwa alama 12 zaidi kuliko Olympique Marseille baada ya kivumbi hicho kutamatishwa ghafla mwishoni mwa Aprili 2020 kutokana na janga la corona.