PSG na Marseille waumiza nyasi bure katika Ligi Kuu ya Ufaransa

PSG na Marseille waumiza nyasi bure katika Ligi Kuu ya Ufaransa

Na MASHIRIKA

OLYMPIQUE Marseille na Paris Saint-Germain (PSG) waliambulia sare tasa katika mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) iliyowakutanisha uwanjani Orange Velodrome.

Mchuano huo ulishuhudia maamuzi mengi yakifikiwa baada ya kurejelewa kwa teknolojia ya VAR huku mashabiki wakitishia kuzua fujo na vurugu. Mechi hiyo ilisimamishwa kwa muda katika vipindi vyote viwili baada ya mashabiki wa pande zote mbili kurusha chupa za maji na vifaa vingine butu uwanjani Neymar alipokuwa akichanja mpira wa kona.

Kwa mara kadhaa, maafisa wa usalama walilazimika kutumia kofia za plastiki kukwepa kuumizwa na vifaa vilivyotupwa na mashabiki uwanjani. Shabiki mmoja sugu wa nyota Lionel Messi alijitoma uwanjani kwa kasi na kumwekea sogora huyo mikono yake mgongoni katika kipindi cha pili.

Vikosi vyote viwili vilifunga lakini mabao hayo yakafutiliwa mbali na refa baada ya kurejelea VAR. PSG walikamilisha mechi hiyo na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya beki Achraf Hakimi kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea visivyo Cengiz Under.

Bao la Luan Peres wa Marseille aliyejifunga kutokana na krosi ya Neymar Jr wa PSG na goli jingine kutoka kwa Arkadiusz Milik katika kipindi cha kwanza yalikataliwa na VAR kwa madai kwamba wafungaji walicheka na nyavu wakiwa wameotea.

Messi ambaye bado hajafungia PSG bao katika kampeni za Ligue 1, alishuhudia mojawapo ya makombora yake yakigonga mwamba wa lango la Marseille huku Konrad de la Fuente akipoteza nafasi nzuri ya wazi kuzamisha chombo cha PSG mwishoni mwa kipindi cha pili.

PSG ambao hawajapigwa katika mchuano wowote wa Ligue 1 kati ya 11 iliyopita, sasa wanajivunia mwanya wa alama saba zaidi kileleni mwa jedwali.

You can share this post!

Dybala aokoa Juventus kinywani mwa Inter Milan katika gozi...

ODM: Raila si ‘kifaranga’ wa serikali

T L