PSG tayari kumsajili Ronaldo kucheza na Messi

PSG tayari kumsajili Ronaldo kucheza na Messi

PARIS, Ufaransa

Paris Saint-Germain (PSG) imepanga kumsajili Cristiano Ronaldo acheze na Lionel Messi iwapo Kylian Mbappe ataamua kuyoyomea Real Madrid ya ligi kuu nchini Uhispania.

Tayari vigogo hao wa Ligue 1 wameunda safu kali ya ushambuliaji inayojumuisha Neymar, Mbappe na Lionel Messi, lakini wameanza mpango wa kumfuatilia Ronaldo kutokana na uvumi kwamba Mbappe anajiandaa kuondoka.

Mkataba wa sasa wa Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 22 unamalizika mwaka ujao, na huenda akahamia La Liga wakati wowote.

Mawazoni mwa kamati ya kiufundi ya PSG, ni Ronaldo anayeonekana kuwa chaguo tosha la kujaza nafasi mshambuliaji huyo matata.

Mkataba wa Ronaldo kwenye klabu ya Juventus unamalizika mwaka ujao, lakini Mreno huyo mwenye umri wa miaka 36 ameeleza nia yake ya kutaka kuagana na vigogo hao wa Italia.

Habari zaidi zimeeleza kwamba wakati PSG wakiendelea kumfuatilia, kocha Carlo Ancelotti wa Real Madrid anafanya kila juhudi kuhakikisha amrejea pale Santiago Benabeu baada ya kusaidia klabu hiyo kutwaa mataji mbalimbali.

Mbali na PSG na Reald Madrid, kadhalika kuna madai kwamba Manchester City wanapigania saini yake.Iwapo Ronaldo hatajiunga na PSG, itabidi Mauro Icardi ajiunge na Juventus kujumuika na Mwargentina mwenzake Paul Dybala.

Mbali na Messi, PSG tayari imewatwaa Gianluigi Donnarumma, Achraf Hakimi, Georginho Wijnaldum na Sergio Ramos.?Madrid nao wanapigania saini ya Paul Pogba, Antonior Rudiger, Mbappe na Leon Gortzeka, baada ya ujio wa David Alaba.

Wakati huo huo, rais wa Barcelona Joan Laporta amemulaumu mtangulizi wake, Joseph Maria Bartomeu kwa kuiwacha klabu hiyo katika hali ngumu kutokana na deni kubwa la zaidi ya Sh173 bilioni.

Bartomeu alijitetea katika barua ya wazi siku ya Jumamosi , akidai kwamba mikakati ya kifedha ambayo angeweka iwapo asingelazimishwa kujiuzulu mwezi Oktoba ingemruhusu Messi kusalia Barcelona.

“Iwapo tungemwongezea kandarasi Lionel Messi, deni la mishahara lingefikia asilimia 110 ya pato lote, suala ambalo ligi ya La Liga ilikataa kukubali’’.

Messi alitangaza kuondoka katika klabu hiyo katika hotuba iliojawa na hisia wiki iliyopita na kuingia katika kandarasi ya miaka miwili na klabu ya PSG.

“Mishahara yetu inawakilisha asilimia 103 ya pato la jumla la klabu hii, hiyo ni sawa na kati ya asilimia 20-25 zaidi ya washindani wetu,’’ alisema Laporta, akiwa katika kipindi cha pili cha uongozi wake tangu aliposhinda uchaguzi wa mwezi Machi.

‘’Kitu cha kwanza tulichofanya tulipowasili tulilazimika kuomba mkopo, la sivyo tungeshindwa kulipa mishahara. Utawala uliopita ulikuwa na udanganyifu chungu nzima.’’

You can share this post!

Chama cha Kiswahili shuleni Kitengela International ni...

WALLAH: Usimtukane mamba kabla hujauvuka mto