Michezo

PSG waduwazwa na limbukeni Lens katika Ligi Kuu ya Ufaransa

September 11th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIKOSI cha Paris Saint-Germain (PSG) kilianza vibaya kampeni za msimu huu wa 2020-21 katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue) kwa kupokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa limbukeni Lens waliopandishwa ngazi mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20.

Kulikuwa na shaka kuhusu uwezekano wa kutandazwa kwa gozi hilo baada ya wanasoka saba wa PSG ambao ni wanafainali wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kuugua ugonjwa wa Covid-19. Kati ya masogora wa haiba kubwa waliopatikana na virusi vya corona kambini mwa PSG ni washambuliaji Neymar Jr na Kylian Mbappe.

Lens walichuma nafuu kutokana na hali hiyo iliyomelemaza uthabiti wa PSG na wakafungiwa bao la pekee na la ushindi kupitia kwa fowadi Ignatius Ganago aliyemwacha hoi kipa Marcin Bulka katika dakika ya 57.

Mechi hiyo ilichezewa mbele ya mashabiki 5,000 walioruhusiwa kuingia katika uwanja wa nyumbani wa Lens, Bollaert-Delelis.

PSG wametawazwa mabingwa wa Ligue 1 katika kipindi cha misimu minane iliyopita.

Chini ya mkufunzi Thomas Tuchel ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Borussia Dortmund nchini Ujerumani, PSG walikamilisha kampeni za Ligue 1 muhula uliopita kwa alama 12 zaidi kuliko nambari mbili Olympique Marseille.

Mbali na Mbappe, wanasoka wengine tegemeo waliokosa kuunga kikosi cha PSG dhidi ya Lens ni Neymar, Marquinhos, Angel di Maria na Mauro Icardi.

PSG kwa sasa wanajiandaa kuwa wenyeji wa Marseille katika gozi kali litakalowakutanisha ugani Parc des Princes mnamo Septemba 13, 2020.