PSG wamsajili kipa Gianluigi Donnarumma wa Italia bila ada yoyote

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) wamemsajili kipa matata wa timu ya taifa ya Italia, Gianluigi Donnarumma, kwa mkataba wa miaka mitano.

Mlinda-lango huyo mwenye umri wa miaka 22 alisalia mchezaji huru baada ya mkataba wake na AC Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Anaingia katika sajili rasmi ya PSG baada ya kuibuka Mchezaji Bora wa kipute cha Euro kilichotawaliwa na Italia baada ya kuzamisha Uingereza 3-2 kwenye fainali iliyochezewa katika uwanja wa Wembley jijini London mnamo Julai 11, 2021.

Donnarumma alipangua penalti mbili za Uingereza kwenye fainali hiyo.

Kufikia sasa, Donnarumma amechezea timu ya taifa ya Italia mara 33 na amekuwa kipa chaguo la kwanza la kikosi hicho ambacho kwa sasa kinanolewa na kocha Roberto Mancini.

Hadi mkataba wake na AC Milan ulipotamatika, Donnarumma alikuwa amewajibishwa na kikosi hicho katika mechi 251 kwenye mashindano yote. Alichezeshwa na AC Milan kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 16.

Alichezeshwa na AC Milan katika mechi zote isipokuwa moja kwenye kampeni za Serie A mnamo 2020-21 na kusaidia kikosi hicho kurejea katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza tangu 2014 baada ya kukamilisha kampeni za Serie A katika nafasi ya pili.

AC Milan tayari wamemsajili kipa Mike Maignan ambaye ni raia wa Ufaransa kujaza pengo la Donnarumma. Maignan alisaidia Lille kukomesha ukiritimba wa PSG kwa kunyakua taji la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo 2020-21.

Chini ya kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino, PSG walibanduliwa na Manchester City kwenye nusu-fainali ya UEFA mnamo 2020-21. Kikosi hicho kilizidiwa maarifa na Bayern Munich kwa kichapo cha 1-0 kwenye fainali ya 2019-20 jijini Lisbon, Ureno.

Donnarumma anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na PSG muhula huu baada ya kiungo mahiri raia wa Uholanzi, Georginio Wijnaldum, 30, kujiunga nao kutoka Liverpool na beki Sergio Ramos, 35, kusajiliwa baada ya mkataba wake na Real Madrid kutamatika.

PSG wamemsajili pia beki raia wa Morocco, Achraf Hakimi, 22, kutoka Inter Milan kwa mkataba wa miaka mitano.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO