Michezo

PSG washuka hadi nafasi ya tatu jedwalini baada ya kupoteza alama muhimu dhidi ya Lille katika Ligue 1

December 21st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) walipoteza alama muhimu kwa mara ya sita msimu huu kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) baada ya kulazimishiwa sare tasa na Lille mnamo Jumapili.

Kikosi cha kocha Thomas Tuchel kilichokosa huduma za fowadi matata Neymar kilitamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira. Hata hivyo masogora hao walishindwa kusuka pasi safi za mwisho huku wakielekeza kombora moja pekee langoni mwa wenyeji wao.

Jaribio la pekee la Lille langoni mwa PSG katika kipindi cha kwanza ni kombora lililovurumishwa na Kaylar Navas baada ya kupokezwa krosi na Burak Yilmaz.

PSG kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 32 baada ya kuambulia sare mara mbili na kupoteza mechi nne hadi kufikia sasa msimu huu. Ni pengo la alama moja ndilo linatenganisha PSG na viongozi wa jedwali Lille na Olympique Lyon.

Akiadhimisha miaka 22 ya kuzaliwa, chipukizi Kylian Mbappe alisazwa na Tuchel kwenye benchi hadi dakika ya 77. Ingawa hivyo, hakuleta utofauti wowote kambini mwa waajiri wake ambao waliambulia sare tasa kwa mara ya kwanza tangu Mei 2018.

Pindi baada ya Mbappe kuletwa uwanjani, Lille walianza kushambulia sana lango la PSG na nusura beki Presnel Kimpembe ajifunge kutokana na presha ya wenyeji wao.

PSG kwa sasa wanajiandaa kuwaalika Strasbourg mnamo Disemba 23 huku Lille wakiwaendea Montpellier.