PSG watumia mabilioni ya pesa kushawishi Mbappe kuwaruka Real Madrid

PSG watumia mabilioni ya pesa kushawishi Mbappe kuwaruka Real Madrid

Na MASHIRIKA

MVAMIZI Kylian Mbappe, 23, ataendelea kusakatia Paris Saint-Germain (PSG) hadi mwaka wa 2025 baada ya kutupilia mbali ofa ya kujiunga na Real Madrid ya Uhispania.

Nyota huyo wa zamani wa AS Monaco amerefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa PSG katika mpango uliogharimu Sh78 bilioni. Sh38 bilioni kutokana na fedha hizo ni bonasi ambazo Mbappe atapokezwa kwa kutia saini mkataba mpya.

Aidha, mshindi huyo wa Kombe la Dunia mnamo 2018 atakuwa akitia mfukoni ujira wa Sh13.3 bilioni kwa mwaka baada ya kutozwa ushuru.

Vinara wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) wameutaja mpango huo kati ya PSG na Mbappe kuwa “kashfa” na sasa wametishia kuwasilisha malalamishi kwa Uefa pamoja na mamlaka husika ya soka nchini Ufaransa na bara Ulaya.

“Kandarasi za aina hii zinatishia ustawi na maendeleo ya kiuchumi ya soka ya Ulaya kwa kuwa mamia ya maelfu ya nafasi za ajira na uadilifu katika soka unakabiliwa na hatari ya kutoweka kabisa,” ikasema sehemu ya taarifa ya La Liga.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Ufaransa na Uhispania, PSG walikuwa radhi kutumia Sh18 bilioni hapo awali ili kumshawishi Mbappe kusalia kambini mwao kwa miaka mingine miwili.

Hata hivyo, kufichuka kwa maafikiano ya siri kupitia kwa wakala Fayza Lamari, kuwa sogora huyo angehamia Real mwishoni mwa msimu huu, kulichochea maamuzi hayo ya PSG waliopepeta Metz 5-0 katika mchuano wa mwisho wa msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Mbappe alipachika wavuni mabao matatu katika pambano hilo lililoshuhudia Metz wakishuka ngazi. Hivyo, aliibuka mfungaji bora wa Ligue 1 muhula huu kwa magoli 28, matatu zaidi kuliko Wissam bne Yerder wa Monaco. Alichangia pia magoli 17 kutokana na mechi 35 huku PSG wakitawazwa wafalme wa Ligue 1 zikisalia michuano minne zaidi.

Mbappe amesema “anafurahia kusalia PSG” huku rais wa kikosi hicho, Nasser Al-Khelaifi, akitangaza kuondoka kwa mvamizi raia wa Argentina, Angel di Maria, anayetarajiwa kuyoyomea Italia kuvalia jezi za Juventus.

“Naamini nitazidi kujikuza kitaaluma nikiwa mchezaji wa PSG. Malengo yangu ni kufikia upeo wa usogora nikiwa nchini Ufaransa nilikozaliwa na kupokezwa malezi ya soka,” akasema Mbappe.

Mbappe alitokea Monaco kwa mkopo mnamo Agosti 2017 kabla ya PSG kumsajili kwa Sh20 bilioni. Tangu wakati huo, ameshindia miamba hao mataji manne ya Ligue 1 katika kipindi cha misimu mitano.

Ingawa alifunga mabao mawili dhidi ya Real kwenye hatua ya 16-bora katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu, waajiri wake walidenguliwa kwa jumla ya mabao 3-2.

Rais wa La Liga, Javier Tebas amekuwa mkosoaji mkuu wa mbinu za PSG na Manchester City kumwaga sokoni mabilioni ya pesa kila msimu kwa minajili ya kujisuka upya.

Kwa mujibu wa Javier Tebas ambaye ni rais wa La Liga, “hatua ya PSG kutumia mabilioni ya pesa kushawishi Mbappe kusalia ugani Parc des Prince baada ya kumwaga sokoni zaidi ya Sh78 bilioni katika misimu ya hivi karibuni ili kujisuka upya licha kukadiria hasara ya Sh35 bilioni mnamo 2020-21, ni “matusi yanayodhalilisha hadhi ya soka”.

“Al-Khelaifi ni hatari kama kipute kipya cha European Super League (ESL) alichounga mkono mwanzoni mwa msimu,” akaongeza Tebas.

Real na Barcelona ni miongoni mwa vikosi 12 vilivyojiondoa haraka kwenye ESL mnamo Aprili huku PSG na Bayern Munich ya Ujerumani wakishabikia kuasisiwa kwa kivumbi hicho kipya.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo akosa njia, Azimio wamtarajia

Desai FC yabwaga Kitisuru Allstars huku Kibagare Slums...

T L