Michezo

PSG wazamisha Lyon katika fainali ya French League Cup na kutia kapuni taji la tatu msimu huu

August 1st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

PARIS Saint-Germain (PSG) waliwafunga Olympique Lyon penalti 6-5 na kutia kapuni ubingwa wa French League Cup mnamo Ijumaa usiku uwanjani Stade de France katika gozi lililohudhuriwa na takriban mashabiki 5,000.

Ufanisi huo uliwashuhudia PSG wakinyanyua jumla ya mataji matatu katika kampeni za msimu mmoja kwa mara ya nne chini ya kipindi cha miaka sita.

Kipute hicho cha French League Cup kilikuwa cha mwisho katika historia baada ya vinara wa soka wa Ufaransa kufikia maamuzi ya kufutilia mbali kivumbi hicho baada ya muhula huu. Maamuzi hayo yalikuwa zao la kikao cha Septemba 2019 kilichowashirikisha washikadau wote wa soka nchini Ufaransa.

Mshindi wa fainali ya msimu huu aliamuliwa kupitia mikwaju ya penalti baada ya pande zote mbili kuambulia sare tasa mwishoni mwa dakika 120.

Baada ya penalti 10 za kwanza kuchanjwa, kipa Keylor Navas wa PSG alipangua kombora Bertrand Traore kabla ya PSG kufungiwa penalti ya ushindi kupitia kwa Pablo Sarabia.

Mechi hiyo ilikuwa ya pili katika soka ya Ufaransa tangu kutamatishwa ghafla kwa kipute cha Ligi Kuu (Ligue 1) mnamo Aprili 2020 kutokana na janga la corona. PSG walitawazwa wafalme wa French League Cup wiki moja baada ya kuwachabanga Saint-Etienne 1-0 na kutia kibindoni ufalme wa French Cup. Fowadi mzawa wa Brazil, Neymar Jr, aliwafungia PSG bao la pekee na la ushindi katika fainali hiyo ya Julai 24.

Lyon walikamilisha mchuano wao wa French League Cup wakiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya beki Rafael Pereira da Silva kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha ziada kwa kosa la kumkabili visivyo fowadi wa PSG, Angel Di Maria nje ya kijisanduku.

Lyon kwa sasa wapo katika hatari ya kukosa kunogesha soka ya bara Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 1996-97 iwapo watakosa pia kunyanyua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Chini ya mkufunzi Rudi Garcia, Lyon kwa sasa wanajiandaa kurudiana na Juventus kwenye mchuano wa mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo Ijumaa ijayo. Watajibwaga ugani kwa gozi hilo wakijivunia ushindi wa 1-0 waliousajili katika mchuano wa mkondo wa kwanza.

PSG ambao kwa sasa wametia kibindoni mataji 25 kati ya 36 yaliyopita katika soka ya Ufaransa, wamepangiwa kuvaana na Atalanta katika robo-fainali ya UEFA mnamo Jumatano ya Agosti 12 kadri wanavyojipania kutia kapuni jumla ya mataji manne katika kampeni za msimu huu.

Hata hivyo, PSG watakosa huduma za fowadi chipukizi Kylian Mbappe dhidi ya Atalanta baada ya Mfaransa huyo kupata jeraha baya la kifundo cha mguu wa kulia wakati wa fainali ya French Cup dhidi ya St-Etienne.

Mbappe anatarajiwa kurejea kutambisha PSG katika soka ya UEFA mnamo Agosti 18, 2020 iwapo watapita mtihani wa Atalanta jijini Lisbon.

Mapambano yote ya robo-fainali, nusu-fainali na fainali ya UEFA yatachezewa jijini Lisbon, Ureno.

Mechi zote za robo-fainali zitaanza kupigwa Agosti 12 katika uwanja Jose Alvalade. Nusu-fainali zitaandaliwa kati ya Agosti 18-19 uwanjani Sport Lisboa Benfica kabla ya uga huo kuwa mwenyeji wa fainali mnamo Agosti 23.

Msimu mpya wa 2020-21 wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) umeratibiwa pia kuanza rasmi mnamo Agosti 23.