Na MASHIRIKA
PARIS Saint-Germain (PSG) walitoka nyuma na kukung’uta Saint-Etienne 3-1 katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).
Ushindi huo uliwezesha PSG kufungua mwanya wa alama 12 kileleni mwa jedwali la Ligue 1.
Baada ya bao la Neymar kufutiliwa mbali kwa madai kwamba alikuwa ameotea, St Etienne walichukua uongozi kupitia Denis Bouanga katika dakika ya 23.
Timothee Kolodziejczak wa St Etienne alionyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza kwa kosa la kumkabili Kylian Mbappe visivyo naye Marquinhos akasawazishia PSG kutokana na mpira wa ikabu katika dakika ya 45.
Angel di Maria aliwaweka PSG uongozini katika dakika ya 79 kabla ya Marquinhos kufunga goli la tatu sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.
Bao la Bouanga lililohesabiwa baada ya kurejelewa kwa teknolojia ya VAR, ilikuwa mara ya 11 kwa PSG ya kocha Mauricio Pochettino kuwa ya kwanza kufungwa katika mchuano wa Ligue 1 mnamo 2021. Hiyo ni rekodi mbaya zaidi kwa miamba hao tangu 2012.
Mechi dhidi ya St-Etienne iliwapa PSG fursa ya kuwajibisha beki Sergio Ramos kwa mara ya kwanza tangu beki huyo raia wa Uhispania ajiunge nao kutoka Real Madrid mwishoni mwa msimu wa 2020-21.
Lionel Messi aliyechangia mabao yote matatu ya PSG, alipoteza nafasi nyingi za kufunga licha ya kuandaliwa pasi za uhakika na Neymar.
PSG kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la Ligue 1 kwa alama 40 huku Rennes wakikamata nafasi ya pili kwa pointi 28.
MATOKEO YA LIGUE 1 (Jumapili):
Saint-Etienne 1-3 PSG
Bordeaux 1-2 Brest
Lorient 0-2 Rennes
Monaco 1-1 Strasbourg
Reims 1-0 Clermont
Montpellier 0-1 Lyon
Marseille 1-0 Troyes
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO