Michezo

PSG yakwamilia malipo ya Mbappe Sh11 bilioni

May 31st, 2024 2 min read

PARIS, Ufaransa

Unaweza kufanyia nini Sh11 bilioni nchini Kenya?

Huo ndio mshahara wa mwezi Aprili ambao Paris Saint-Germain wanasemekana hawajalipa Kylian Mbappe kutokana na mvutano kati ya pande hizo mbili wakati supastaa huyo anajiandaa kuhama mabingwa hao wa Ufaransa.

Uamuzi wa PSG kukwamilia mshahara wa Mbappe unaaminika kutokana na makubaliano walifanya mwanzo wa msimu 2023-2024 mwaka jana wakati mshambulizi huyo alikubali kupunguzwa bonasi anayofaa kupata.

Ripoti zinadai kuwa PSG na Mbappe wanafanya mazungumzo na wanatarajia kuelewana.

“Kila kitu kinashughulikiwa,” ripoti zilinukuu mdokezi bila ya kuthibitisha kiasi cha fedha ambacho Mbappe anadai.

Hata hivyo, mdokezi mwingine anasema kuwa PSG pia iliamua haitamlipa Mbappe malimbikizi ya marupurupu kumaanisha kuwa kiasi nahodha huyo wa Ufaransa anafaa kupokea ni karibu Sh11.2 bilioni jinsi gazeti la L’Equipe liliripoti hapo awali.

Mdokezi huyo anasema kuwa PSG iliamua kutofanya malipo bila ya kuonya Mbappe na pia makubaliano kati yao.

Kandarasi ya Mbappe, 25, itakatika Juni 30 na tayari amethibisha kuwa ataondoka PSG baada ya kuitumikia kwa miaka saba, huku akihusishwa na kuhamia Real Madrid.

Kambi hizo mbili zilikiri mwanzo wa mwaka huu kuwa Mbappe alikubali kupunguza sehemu ya marupurupu yake makubwa aliyofaa kulipwa ili apate kujumuishwa tena katika kikosi cha PSG baada ya kuachwa nje mwanzoni mwa msimu.

Inaaminika malimbikizi ya bonasi hizo ni kati ya Sh8.4 bilioni na Sh9.8 bilioni.

Kukubali kupunguzwa kiasi hicho kulionekana kama njia ya Mbappe kusaidia PSG kutotoka mikono mitupu kwa sababu PSG haitapokea ada ya uhamisho akiondoka.

Hata hivyo, mdokezi mwingine anadai kuwa Mbappe alishapata bonasi yake mwezi Februari.

Mbappe alijiunga na PSG mnamo Agosti 2017 akitokea AS Monaco na kusaini kandarasi yake ya mwisho na mabwanyenye hao mwaka 2022 alipoamua kuwatumikia kwa miaka mingine miwili akipata mshahara wa Sh10.1 bilioni kabla ya kutozwa ushuru.

Juu ya hiyo kulikuwa na ada ya kusaini kandarasi ya Sh21.1 bilioni ya kulipwa kidogo kidogo, pamoja na bonasi ya uaminifu kwa mwaka wa kwanza ya Sh9.8 bilioni na Sh11.2 bilioni kwa mwaka wa pili.

Isitoshe, Mbappe angepata Sh12.7 bilioni kwa mwaka wa tatu kama angeamua kurefusha kandarasi kwa mwaka mwingine.