PSG yapepeta Lyon kwenye mechi ya kwanza ya Messi katika uwanja wa nyumbani

PSG yapepeta Lyon kwenye mechi ya kwanza ya Messi katika uwanja wa nyumbani

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alichezeshwa na Paris Saint-Germain (PSG) kwa mara ya kwanza katika uwanja wa nyumbani wa Par des Princes ila akatolewa ugani katika kipindi cha pili cha mchuano huo ulioshuhudia wenyeji wakisajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Olympique Lyon.

Messi aliyeingia katika sajili rasmi ya PSG muhula huu, alishuhudia makombora yake mawili yakigonga mwamba na mhimili wa goli la Lyon kabla ya fataki zake nyingine mbili kupanguliwa na kipa Anthony Lopes.

Matokeo yakiwa 1-1, Messi aliondolewa na nafasi yake kutwaliwa na beki Achraf Hakimi. Japo Messi alipigiwa makofi na mashabiki, alionekana kutofurahia maamuzi ya kutolewa ugani.

Nyota huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 34, aliagana na Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2020-21. Baada ya kuondoka ugani, hakusimama tena kutazama wenzake uwanjani ila akamnong’onezea kocha Mauricio Pochettino jambo fulani.

Mauro Icardi ambaye pia aliingia uwanjani katika kipindi cha pili, ndiye aliyefunga bao la ushindi kwa upande wa PSG baada ya kukamilisha krosi ya Kylian Mbappe kwa ustadi.

Awali, Lucas Paqueta alikuwa amefuma wavuni mpira aliopokezwa na Karl Toko Ekambi na kuwapa Lyon uongozi. Neymar alisawazishia PSG katika dakika ya 66 baada ya kuchezewa visivyo na beki chipukizi wa Lyon, Malo Gusto.

Mechi dhidi ya Lyon ilikuwa ya tatu kwa Messi kuchezea PSG na ya tatu kwa supastaa huyo kuwahi kuchezea kikosi kingine tofauti mbali na Barcelona.

Ilimchukua Messi siku 40 kuwajibikia PSG nyumbani kwa sababu ya kushuka kwa fomu ya ubora wa makali yake pamoja na likizo fupi iliyoshuhudia ligi mbalimbali zikisitishwa ili kupisha michuano ya kimataifa.

Mchuano wa kwanza kwa Messi kuwajibikia PSG ulikuwa dhidi ya Reims waliochabangwa 2-0. Messi alitokea benchi katika mechi hiyo baada ya Mbappe kupachika wavuni mabao yote mawili ya PSG.

Alipangwa katika kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 15, 2021 katika sare ya 1-1 iliyosajiliwa na PSG dhidi ya Club Bruges ya Ubelgiji kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Sawa na hali ilivyokuwa dhidi ya Lyon; Messi, Mbappe na Neymar walianzishwa katika mchuano kati ya PSG na Lyon na wakawa tegemeo la PSG katika safu ya mbele.

Mchuano ujao wa PSG ni dhidi ya Metz ugenini mnamo Septemba 22, 2021. Ni mechi ambayo PSG wanatazamiwa kutumia kama jukwaa la kuwavunia ushindi wa saba mfululizo katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kilio wageni wakiwadhulumu watoto kingono Pwani bila kujali

Njaa: Serikali kuanza kusambaza mlo, maji