Habari za Kaunti

Punda wakamatwa kwa kufunza watoto tabia mbaya

February 14th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAMILIKI wa punda ambao huwaachilia wanyama hao kurandaranda ovyo mitaani kisiwani Lamu huenda wakaanza kuadhibiwa kwa kupigwa faini endapo watashindwa kuwadhibiti wanyama kusalia sehemu pamoja.

Hii ni kutokana na malalamishi kwamba punda wa kurandaranda mitaani wamekuwa wakiharibu mpangilio wa mji wa kale wa Lamu na ule wa Shella, ambayo yote miwili ni vivutio vikuu vya watalii.

Walalamishi wanadai kwamba punda hao huangusha kinyesi onyoovyo, hivyo kuchafua mazingira.

Viongozi na maafisa wa baraza la mji wa kisiwa cha Lamu pia wamelalamikia tabia ya punda kujamiiana hadharani, hali ambayo wanahisi inawafunza watoto tabia mbaya.

Kufikia juma hili, makumi ya punda tayari walikuwa wamekamatwa mjini Shella na kutiwa alama maalum ya utambulisho, ambapo wenye punda watahitajika kufika katika ofisi za baraza la mji wa Lamu kueleza sababu za kwa nini waliwaachilia punda wao kurandaranda ovyo na kuharibia watalii na wenyeji amani yao.

Punda wa kurandaranda mitaani wakila taka katika dampo mojawapo Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Meneja wa Baraza la Miji ya Kisiwa cha Lamu, Abdulswamad Abdalla, alilalamikia hatua ya serikali ya kaunti kulipa fedha nyingi kila kuchao kwa vibarua kusafisha miji, hasa ule wa kale wa Lamu, na Shella.

“Uchafu wenyewe unaosafishwa, asilimia kubwa huwa ni kinyesi cha punda. Kwa nini kaunti ilipe watu kusafishia punda kinyesi? Tumeanza harakati za kuwakamata na kuwatia vibandiko hawa punda,” akasema Bw Abdalla.

Meneja wa Manispaa ya Baraza la Miji ya Kisiwa cha Lamu, Abdulswamad Abdalla. Anasema hairidhishi kaunti kuendelez kupewa mzigo wa kukodisha watu kusafisha kinyesi cha punda mitaani, hivyo kuna haja ya punda wa kurandaranda ovyo kudhibitiwa. PICHA | MAKTABA

Pia aliongeza kwamba wako mbioni kuzungumza na jamii kuafikiana ni adhabu au faini gani atapokea mwenye punda kwa kumuachilia mnyama wake kurandaranda ovyo na kuchafua mazingira kwenye “miji yetu ya kitalii”.

“Punde hilo likipitishwa, basi wenye punda wataanza kulipa faini,” akaongeza.

Diwani wa wadi ya Shella Atwa Salim, aliweka wazi kuwa kamwe hapendezewi na tabia ya punda wanaorandaranda mitaani, kufukuzana ovyo vichochoroni na majumbani, ambapo huishia kujamiiana hata mbele ya watoto.

Diwani wa wadi ya Shella Atwa Salim. Bw Salim anashikilia kuwa punda wanaorandaranda mitaani hupotosha maadili ya jamii kutokana na tabia ya wanyama hao kujamiiana hadharani. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Salim anasema kamwe hataruhusu maadili ya jamii ya Lamu, hasa wakazi wanaoishi mji wa kale wa Lamu na Shella kupotoshwa kupitia vitendo vya hayawani hao.

“Punda warandaji wamekuwa kero kwa masikio yetu na hata kimaadili. Unapata punda wanapiga kelele kila mahali usiku na mchana na kutukosesha amani. Wengine wanafukuzana na kisha kujamiiana hadharani watoto wa shule na wale wachanga kabisa wakitazama. Hilo linaleta fikra potovu kwa kizazi chetu kichanga. Lazima mikakati kabambe iwekwe  kudhibiti hawa hayawani,” akasema Bw Salim.

Kwa upande wao aidha, watetezi wa Haki za Punda kisiwani Lamu wameshinikiza kuwepo na umakinifu katika kuwadhibiti punda, hasa wale wanaorandaranda mitaani bila ya haki zao kukiukwa.

Afisa Msimamizi wa Kituo cha Matibabu ya Punda kisiwani Lamu Obadiah Sing’oei, alieleza kutoridhishwa kwake na hatua ya hivi majuzi, ambapo punda wanaorandaranda mjini Shella walikamatwa na kisha kufungiwa katika sehemu fulani ya taka.

“Utakamataje punda na kisha kumfungia mahali pa kutupa taka kwa saa kadhaa. Huo ni ukiukaji mkubwa wa haki za wanyama. Hawa punda wetu wamekuwepo tangu jadi hapa Lamu na jamii haijalalamika. Huku wakiibuka na sheria ya kudhibiti punda wanaorandaranda mitaani, pia nitasisitiza jamii ihusishwe kikamilifu na pia haki za hao punda ziheshimiwe vilivyo,” akasema Bw Sing’oei.

Afisa Msimamizi wa Kituo cha Matibabu ya Punda Lamu Obadiah Sing’oei akiwa ofisini mwaka ambapo alisisitiza haja ya haki za punda kuheshimiwa, hata wale wanaorandaranda mitaani. PICHA | KALUME KAZUNGU

Punda ni kiungo muhimu kwa usafiri wa binadamu na mizigo kwenye visiwa mbalimbali vya Kaunti ya Lamu.

Mji wa kale wa Lamu ambapo usafiri wa magari, pikipiki na baiskeli hauruhusiwi, utapata karibu punda 3000 wakihudumu ndani ya kisiwa hicho pekee.

Ni kwenye mji wa kihistoria wa Lamu ambapo punda pia huenziwa zaidi kushinda hata magari au vyombo vingine vyovyote vya usafiri.

Hii ndio sababu kila familia ambayo asili yake ni Lamu, inamiliki punda.

Punda wakirandaranda kisiwani Lamu. Wamiliki wa punda huenda wakapigwa faini mjadala wa kukamata punda warandaji mitaani ukipitishwa. PICHA | KALUME KAZUNGU