Putin ataja maeneo 4 Ukraine kuwa ya Urusi

Putin ataja maeneo 4 Ukraine kuwa ya Urusi

NA MASHIRIKA

KYIV, Ukraine

URUSI imedai kuwa raia wa maeneo ambayo imeteka kutoka Ukraine, wamepitisha kura ya kuwa raia wa Urusi, huku Ukraine na washirika wake wakishtumu hatua hiyo kama ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Kulingana na Urusi, maeneo hayo manne ya Donetsk, Luhansk, Zaporizhia ana Kherson, ambayo kwa jumla ni asilimia 15 ya Ukraine, sasa ni sehemu ya Urusi.

Maafisa wa Luhansk wanaoungwa mkono na Urusi walitangaza kuwa asilimia 98 ya wakazi walipiga kura ya kujiunga na Urusi, Zaporizhia asilimia 93, Kherson asilimia 87 na Donetsk asilimia 99.

Kura hiyo ya maoni ilifanyika nyumba kwa nyumba katika kile Ukraine imetaja kama shughuli iliyoendeshwa kimabavu katika njama ya Urusi ya kuteka maeneo yake.

Wadadisi wanasema Rais Vladimir Putin wa Urusi sasa atatumia kisingizio kuwa mashambulizi katika maeneo hayo ni uvamizi wa ardhi yake.Wiki iliyopita Putin alitishia kutumia silaha za nyuklia kulinda ardhi ya Urusi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliandaa kikao mnamo Jumanne kujadili hatua ya Urusi kudai maeneo hayo manne kuwa sehemu yake.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alihutubia kikao hicho, ambapo alidai wakazi wa maeneo hayo walikuwa wakilazimishwa kupiga kura ya kujiunga na Urusi “wakiwa wameshikiwa bunduki”.

Zelenskyy alisema hatua ya Urusi kuendelea kuteka maeneo yake kunazamisha juhudi zozote za mazungumzo ya amani na Urusi, ambayo ilivamia Ukraine mnamo Februari.

Kura ya kujiunga na maeneo hayo iliandaliwa kwa dharura baada ya majeshi ya Ukraine kuwatimua wanajeshi wa Urusi katika baadhi ya maeneo kusini mwa taifa hilo.

Washirika wa Ukraine walishutumu utekaji wa maeneo hayo huku Canada ikitangaza kuwa itaweka vikwazo vipya dhidi ya Urusi.

“Canada kamwe haitambui matokeo ya kura haramu ya maoni ama jaribio la Urusi kuteka maeneo ya Ukraine. Naweka wazi kuwa mipaka ya Ukraine haitabadilika,” akasema waziri mkuu wa Canada, Justin Trudeau.

Wakati huo huo, wanaume wanaendelea kutoroka nchini Urusi kuepuka kulazimishwa kujiunga na wanajeshi wanapopigana dhidi ya Ukraine.

Hali hiyo imekuwa ikiendelea tangu Putin alipoagiza wanaume walio na uwezo wa kupigana kujiunga na jeshi.

  • Tags

You can share this post!

Mombasa yabaki kwa mataa ikikosa vitamu vya Ruto

Maonyesho ya kilimo na biashara yanoga jijini Nairobi

T L