Pwani: Kuna haja wazazi, serikali kulinda watoto dhidi ya uhalifu mtandaoni

Pwani: Kuna haja wazazi, serikali kulinda watoto dhidi ya uhalifu mtandaoni

NA ALEX KALAMA 

WATOTO wengi eneo la Pwani wameathirika zaidi na utumizi mbaya wa mtandao huku kaunti za Mombasa, Kilifi na Lamu zikiwa ndizo zinaongoza kwa idadi hiyo.

Haya ni kwa mujibu wa idara ya watoto eneo la Pwani ambayo imeeleza kuwa serikali imeanzisha hamasisho ili kuwanusuru watoto wajiepushe na matumizi mabaya ya mitandao.

Kulingana na mshirikishi wa idara ya watoto eneo la Pwani George Migosi ipo haja ya hamasa zaidi kutolewa kwa wazazi ili waweze kuwalinda wana wao kutokana na wahalifu wanaowawinda watoto wadogo mitandaoni.

Akizungumza na wanahabari mjini Kilifi Migosi amesema kaunti ya  Mombasa inaongoza katika idadi ya watoto wanaotumia mitandao vibaya na hatimaye kuishia kuhujumiwa haki zao.

“Kisiwa cha Mombasa kile kimeathirika sana ukija Kilifi upande wa Mtwapa,Watamu,Malindi na hata Lamu imeanza kuathirika na hii mambo ya mitandao.

Lakini wale wazazi wameachilia watoto wao wanaharibika kupitia kwa mitandao ni hao wazazi ambao hawasomi tena,” alisema Bw Migosi.

Naye mkurugenzi wa shirika la Terre Des Hommes Netherlands linalojishughulisha na haki za watoto Magdaline Muoki ameeleza kuwa ipo haja ya serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wanaodhulumu watoto kupitia mitandao.

Hata hivyo ameitaka serikali kuweka mikakati ya thabiti kuhakikisha kuwa sheria zilizoko za kuwalinda watoto zinafuatwa vilivyo.

“Kweli kuna wale ambao wanadhulumu watoto lakini wako wapi? Hatuwaoni wakipelekwa mahakamani. Tunataka tushirikiane na serikali hususan idara ya polisi ili tuone kama wanaweka mikakati ya kuangalia ni wapi wanaweza enda ama ni vipi wanaweza kuwakamata wahalifu. Jambo la pili kuna hili ambalo umesikia serikali inataka kuzindua… Mkakati wa Serikali Kulinda Watoto yaani ‘National plan of Action on Child Protection’. Tunajua Kenya iko na sheria nyingi sana ambazo zimewekwa ili kuweza kuwalinda watoto, lakini changamoto kuu ni namna ambavyo sheria hizo zinaweza kufanya kazi,” alisema Bi Muoki.

Aidha Wanjala Blasio kutoka shirika la kimataifa la USAID kwa upande wake alieleza kuwa ipo haja ya sheria zilizopo za kuwalinda watoto kufanyiwa marekebisho ili ziweze kupambana na uhalifu wa mitandaoni katika karne ya sasa.

“Ukiangalia matumizi ya mitandao na zile sheria ambazo ziko za kulinda watoto bado hazijafika, matumizi ya mitandao iko mbele sheria bado zinang’ang’ania kufikia yale matumizi na utandawazi ulioko. Kwa hivyo labda ningehimiza serikali ya kaunti na serikali ya kitaifa kupitia bunge waweze kubuni na kueka mikakati na sheria ambapo zitahakikisha kuwa mtoto analindwa katika matumizi ya mitandao,kwa sababu lazima watoto watatumia mitandao,” alisema Bw Blasio.

  • Tags

You can share this post!

Tetemeko: Phoebe Oketch athibitisha yeye na wenzake 2 wa...

TAMTHILIA: Mtiririko wa matukio katika Sehemu ya I, Onyesho...

T L