Habari MsetoSiasa

PWANI: Siasa za viuno zilivyotenganisha Jumwa na Mboko

November 19th, 2018 2 min read

NA MOHAMED AHMED

MGAWANYIKO mkubwa umezuka kati ya wanawake wawili maarufu kisiasa katika eneo la Pwani, Aisha Jumwa na Mishi Mboko kuhusu ni nani wa kumuunga mkono kuwa rais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Huku Bi Mboko, ambaye ni Mbunge wa Likoni akisisitiza kuwa bado ni mfuasi sugu wa ODM, Bi Jumwa (Malindi) amejitoza wazi na kutangaza kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto. Na wanasiasa hao sasa wanapapurana hadharani kwa kutumia silaha kali waliojaliwa nayo: Semi na mafumbo.

Wawili hao wana ujuzi wa kutumia kinaya na kejeli tele katika maneno yanayosisimua wafuasi wao na kuwakwaza wapinzani wao. Hii ni kati ya sababu urafiki wao ulishamiri, hususan, wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Kunawiri kwa usuhuba wao kulijitokeza zaidi katika mtindo wao wa kumuandama kwa cheche za maneno yeyote aliyejaribu kudunisha chama chao cha ODM.

Na mwathiriwa mkuu wa kejeli za wabunge hawa machachari ambao wanasifika eneo la Pwani kama “masimba jike” ni aliyekuwa seneta wa Mombasa, Hassan Omar ambaye walimwangushia makombora huku, kwa weledi mkubwa, wakikejeli umbo lake.

Lakini sasa, urafiki wa viongozi hao wawili umeonekana kusambaratishwa na maneno hayo hayo ya mafumbo ambayo wamebobea kwayo.

Kwa sasa, siasa za mafumbo ya viuno baina ya wawili hao zinaonekana kunogoa na kuzua mwanya mkubwa baina yao.

“Sisi hatuna biashara ya kuuza viuno katika cha ODM. Huku tunaauza sera na maendeleo. Kuna wale ambao wanauza viuno na tunawambia wanajua maskani ya kuuzwa viono ni wapi,” akasema Bi Mboko wiki iliyopita katika sherehe moja eneo la Changamwe.

Matamshi ya Bi Mboko yalitiliwa mkazo na rafikite wake aliyechukuwa nafasi yake ya awali ya kiti cha mwakilishi wa wanawake Bi Aisha Hussein.

Bi Hussein alisema: “Msimamo wetu si wa viuno, sisi misimamo yetu ni wa kazi. Kama wataka kuendesha kiuno, peleka biashara hiyo mbele. Sisi ndio masimba wa kike,” akasema Bi Hussein.

Matamshi ya wawili hao yalikuwa yanaelekezwa wazi kwa hasimu wao wa sasa, Bi Jumwa ambaye wakati wa ziara ya mwisho ya Naibu Rais William Ruto katika kanda ya Pwani mwezi jana, alichemsha wakazi Kwale na Mombasa aliposema anaitambua zaidi kazi ya kiuno.