Pwani walisota zaidi Kenya 2020 – Utafiti

Pwani walisota zaidi Kenya 2020 – Utafiti

Na MARY WANGARI

WAKAZI wa eneo la Pwani waliongoza kwa idadi ya Wakenya waliotaabika katika mwaka wa 2020 uliomalizika hivi punde, utafiti umefichua.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Infotrak, eneo la Pwani liliongoza kwa idadi ya watu waliotaja 2020 kama mwaka mgumu kwa asilimia 72.

Eneo hilo hutegemea kwa uchumi wake utalii na usafirishaji mizigo katika bandari ya Mombasa.

Sekta ya utalii ni miongoni mwa zilizoathirika zaidi na kanuni kali zilizopitishwa kwa lengo la kuepusha ueneaji wa maambukizi ya virusi vya corona.

Vile vile, usafirishaji mizigo kimataifa ulipungua kutoka nchi za kigeni hasa katika miezi ya kwanza janga la corona lilipotangazwa nchini mnamo Machi 2020.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa Infotrak iliyotolewa jana, Pwani ilifuatiwa na Nyanza ambapo kulikuwa na asilimia 64 ya watu waliotaja mwaka wa 2020 kuwa mgumu mno, kisha Nairobi (asilimia 62).

“Kuyumbayumba kwa uchumi, kupoteza ajira, kusambaratika kwa biashara, kupoteza marafiki, mwajiriwa mwenza au mpendwa kutokana na Covid-19, kuambukizwa virusi vya corona ni miongoni mwa sababu zilizofanya 2020 kuwa mwaka mgumu,” ikasema sehemu ya ripoti hiyo.

Ukosefu wa ajira ni kati ya sababu kuu zilizotajwa kutatiza wananchi zaidi kwa asilimia 18, ikifuatiwa na gharama kubwa ya maisha (asilimia 13).

Changamoto nyingine kuu zilizotajwa ni ukosefu wa huduma bora ya afya (asilimia 10), ufisadi (asilimia 7) na janga la Covid-19 (asilimia 6).

Kwa jumla, asilimia 95 ya Wakenya waliutaja 2020 kama mwaka uliokuwa mgumu mno huku wengi wao wakiwa na matumaini kwamba hali itakuwa bora mwaka huu.

Utafiti huo ulifanyika kati ya Disemba 27 na Disemba 29 na ulihusisha kaunti 24 na maeneo yote manane nchini Kenya ambapo watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi walihojiwa.

Sherehe

Isitoshe, kulingana na ripoti hiyo, Wakenya 8 kati ya 10 waliashiria kwamba hawakuweza kusherehekea msimu wa sherehe ikilinganishwa na miaka ya awali.

Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa asilimia 95 ambapo wakazi 9 kati ya 10 walishindwa kujumuika na familia na jamaa zao kusherehekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ikilinganishwa na miaka iliyotangulia.

Wengi wao walitaja changamoto za kifedha kama sababu kuu iliyowazuia kusherehekea huku sababu nyinginezo zikiwa juhudi za kujikinga na kulinda familia zao dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona katika maeneo yenye mikusanyiko ya umma na kafyu iliyowekwa na serikali kuanzia saa 10 alfajiri hadi saa nne usiku, mtawaliwa.

Idadi kubwa ya Wakenya wana imani kwamba, uchumi utaimarika na kwamba Kenya itapokea chanjo dhidi ya Covid-19, huku wakazi katika eneo la Kaskazini Mashariki wakiongoza kwa asilimia 70 kwa walio na matumaini kuhusu 2021.

Ni Wakenya wachache mno hata hivyo, katika asilimia moja, walio na matumaini kwamba kutakuwa na kura ya maoni itakayobadilisha utawala nchini Kenya 2021.

You can share this post!

Viongozi wataka Mvurya avalie joho la Sultan

Chiloba sasa apata kazi serikalini baada ya kutimuliwa na...