Habari

Pwani wasaka dawa ya corona mitini

April 13th, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

WAKAZI katika maeneo tofauti ya Pwani wameanza kutumia dawa za miti-shamba wakiamini zitawakinga wasiambukizwe virusi vya corona.

Haya yamefichuka siku chache baada ya uvumi mwingine kuenea Pwani na kusisimua wengi kwamba chai ya rangi bila sukari ni kinga dhidi ya corona.?Mbinu hizo hazijathibitishwa kisayansi kuweza kukinga wala kuponya ugonjwa huo ulioangamiza maelfu ulimwenguni.

Wataalamu wanasema uenezaji wa imani hizo za kitamaduni unatishia kuvuruga vita dhidi ya maradhi hayo.

Tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona nchini China mnamo Desemba mwaka uliopita, wanasayansi hawajafanikiwa kupata dawa wala chanjo dhidi yake.

Bw Hassan Mohammed kutoka eneo la Kizingo, wadi ya Tiwi, Kaunti ya Kwale alisema mababu zao walitumia miti-shamba kupigana na maradhi mbalimbali ikiwemo ukambi na homa.

“Kuna miti kama murubaini, mzunje, vumbamanga, mmachomacho, mrehani na mtseketse ambayo wazee wetu walitumia kujitibu na kuimarisha kinga ya miili yao. Tumeamua kutumia dawa za asilia kupambana na ugonjwa huu wa corona,” akasema Bw Mohammed.

Mkazi mwingine Bi Asha Mgayu, alisema japo wanafuata masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya kama vile kunawa mikono na kuepuka maeneo yenye watu wengi, wameamua kupiga hatua zaidi kukabiliana na virusi hivyo kwa kujitafutia kinga za kiasili.

“Mwarubaini unaaminika kuwa tiba ya magojwa 40 na ni maarufu sana kote duniani, kinyume na dawa za kutengenezwa katika maabara. Dawa za kienyeji hazina madhara yoyote,” akasema.

Katika Kaunti ya Kilifi, Mwenyekiti wa Chama cha Utamaduni wa Mijikenda Joseph Mwaradandu, alidai kuwa katika miaka ya 1950s, ugonjwa wenye dalili sawa na virusi vya corona uliwakumba wakazi wa Pwani.

Kulingana naye, ugonjwa huo uliofahamika kama kivuti, uliathiri viungo vya mwanadamu vya kupumua jinsi corona inavyofanya.?Alieleza kuwa mgonjwa aliyeugua kivuti alipata matatizo ya kupumua, kikohozi kikavu na kupatwa na joto kali mwilini.

Sawa na ilivyo kwa Covid-19, mgonjwa wa kivuti alitengwa na jamii ili kuepusha maambukizi, kisha kufanyiwa matibabu kwa kutumia miti-shamba.

Kwa msingi huu, aliitaka serikali iwazie kushauriana na wataalamu wa miti-shamba ili kupambana na virusi vya corona.

“Kuna baadhi ya watu wanahusisha miti-shamba na uchawi na ushirikina. Huu si uchawi bali ni kutumia miti asilia kutengeza tiba,” alisema Bw Mwarandu.

Bw Mwarandu alisema matibabu yalihusisha kuchemshwa kwa majani ya miti ya mdungu, mhirihiri, mberandu na mwarubaini.

“Baada ya majani hayo kuchemka mgonjwa angeketishwa kwenye kiti karibu na chungu kilichotokosewa majani hayo kisha kufunikwa na nguo zito ambayo hairuhusu moshi kutoka nje,” akasema Bw Mwarandu.

Alieleza kuwa mgonjwa angeachwa kuketi ndani ya nguo hiyo kwa muda wa dakika 20 hadi atoke jasho kisha kutolewa katika zoezi lililojulikana kama cheruko.

“Baada ya kutokwa jasho, mtabibu angetumbukiza kitambaa kwenye jungu la mitishamba kisha kumkanda mgonjwa katika sehemu za mbavu, mgongo na koo,” akaeleza mzee huyo.

Kujikinga na kuambukizwa, anayemuhudumia mgonjwa pia alitengenezewa dawa sawia na ya mgonjwa.

Hayo yanaendelea huku maambukizi yakizidi kuongezeka nchini. Jana, watu sita zaidi walitangazwa kuambukizwa na kufanya idadi kufika 197.

Wanne ni wakazi wa Nairobi, mmoja wa Mombasa na mwingine wa Siaya, ambaye alifariki.

Kufikia jana watu milioni 1.8 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo katika mataifa 210 duniani, nusu milioni kati yao wakiwa wako Amerika.

Amerika pia ilipita Italia kwa idadi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo ikiandikisha vifo zaidi ya elfu 21, nayo Italia ikiwa na elfu 19. Uhispania nayo ni ya tatu kwa elfu 16.