Pwani wasema hawana cha kusherehekea Madaraka Dei

Pwani wasema hawana cha kusherehekea Madaraka Dei

KALUME KAZUNGU na VALENTINE OBARA

VIONGOZI na wakazi wa eneo la Pwani wamelalamikia ukosefu wa mafanikio makubwa eneo hilo, Kenya inapoadhimisha miaka 58 ya uhuru wa kujitawala.

Katika mahojiano na Taifa Leo, walitaja changamoto kama vile uskwota, ukosefu wa ajira na umaskini kuwa miongoni mwa masuala ambayo yanawaletea wengi machozi kila kukicha, huku mabwenyenye wachache wakijaza pesa mifukoni.

Licha ya mabilioni ya pesa kutengewa miradi mikubwa mikubwa, wakazi katika baadhi ya maeneo ya Pwani hutatizika kwa ukosefu wa miundomsingi muhimu kwa maisha ya kila siku kama vile usambazaji maji ya mifereji na mabomba ya kutosha ya kusafirisha majitaka.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa, Hussein Khalid, anasema Wapwani wana machache ya kujivunia kwa vile matatizo yanayokumba umma hayajatatuliwa kwa kiwango cha kuridhisha, licha ya kuwa wengi walitarajia ugatuzi ungeleta mabadiliko.

“Pwani iko nyuma ikilinganishwa na maeneo mengine nchini. Wapwani hawana lolote la kusherehekea. Ufisadi, ukabila katika ajira na umasikini ni mambo ambayo yameharibu hali zaidi,” asema Bw Khalid.

Katika miaka ya hivi majuzi, serikali kuu na za kaunti zilionekana zikijaribu kutatua matatizo hayo ambayo yamekuwepo tangu jadi.

AJIRA KUHAMISHIWA BARA

Hayo yameshuhudiwa kupitia kwa utoaji hatimiliki za ardhi kwa wakazi ambao walikuwa maskwota kwa miaka mingi, na upanuzi wa miundomsingi na rasilimali muhimu kama vile barabara na bandari.

Licha ya haya, kumekuwepo malalamishi kwamba wenyeji wa Pwani bado hubaguliwa katika uajiri hasa katika mashirika ya serikali, huku ujenzi wa miundomsingi kama vile reli ya SGR ukilaumiwa kwa kuhamisha nafasi za kazi kutoka bandari ya Mombasa hadi maeneo ya bara.

Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Mohamed Mbwana, asema watajivunia kuadhimisha au kusherehekea kikamilifu Madaraka Dei ya nchi hii siku ambapo Wapwani watazika uskwota katika kaburi la sahau.

“Nakumbuka punde alipoingia madarakani mwaka wa 2013, Rais Kenyatta alizuru Pwani ambapo alitoa zaidi ya hatimiliki za ardhi 60,000. Amekuwa akijitahidi kutoa hatimiliki karibu kila mwaka. Licha ya hayo yote, tatizo la ukosefu wa ardhi na hatimiliki kwetu sisi Wapwani bado lipo,” asema Bw Mbwana.

Bw Mohamed Athman, ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Haki za Kijamii la Save Lamu, asema inasikitisha jinsi maelfu ya maskwota wa ghasia za majambazi wa Shifta wa mwaka 1963 katika Kaunti ya Lamu hadi sasa hawajapata makao.

Naye mwenyekiti wa bodi ya shirika la kutafiti masuala ya ardhi la Land Development and Governance Institute, Ibrahim Mwathane, aeleza kuwa suala la ardhi Pwani ni kubwa mno na haliwezi kutatuliwa haraka.

Kulingana na Bw Mwathane, changamoto kuhusu umiliki wa ardhi ni tatizo la kihistoria katika ukanda huo kwa hivyo litahitaji miaka mingi kabla wananchi washuhudie afueni hata kama serikali imeeka mikakati.

Suala la ajira pia limekuwa donda dugu Pwani kwa miaka mingi.

Kiongozi wa vijana eneo la Lamu, Michael Kanja anasisitizia haja ya serikali kutatua zogo la ukosefu wa ajira ili kuwaepusha vijana kujiingiza kwenye janga la mihadarati.

Anasema miaka 58 ya uhuru imekuwa ya mateso kwa vijana wengi Pwani, ambapo wengi wamelazimika kuishi kwa umaskini ilhali wengine wakipotelea kwenye uraibu wa dawa za kulevya, wizi na ugaidi kwa kukosa ajira.

“Vijana wa Pwani tuna mambo kidogo sana ya kujivunia. Mengi ni machozi tu. Ajira bado ni changamoto. Mihadarati pia inaendelea kutusonga na kutumaliza. Viongozi wetu watutetee ili nasi tujivunie uhuru wa nchi yetu miaka ijayo,” asema Bw Kanja.

Hata hivyo, Diwani wa Wadi ya Hongwe katika Kaunti ya Lamu, James Komu asema kuwa licha ya matatizo ambayo yangali yapo, wananchi pia wanafaa kutambua hatua za kimaendeleo ambazo Kenya imepiga Pwani.

Bw Komu asema kwa mara ya kwanza tangu uhuru wa Kenya kupatikana, Lamu inaadhimisha Madaraka Dei ikiwa na barabara kuu ya kisasa ya lami ya kilomita 114 ya Lamu – Witu – Garsen.

umekuwa ukiendelea eneo hilo tangu Machi, 2017.

Bw Komu pia alitaja bandari ya Sh 310 bilioni ya Lamu kuwa hatua kubwa ambayo wakazi wa Lamu na Pwani kwa jumla wanajivunia.

“Kwa upande wangu, Madaraka Dei ya mwaka huu 2021 ni ya kipekee na yanayofaa tujivunie kama wakazi wa Lamu. Tumejionea maendeleo, ikiwemo barabara na bandari ya Lamu vikikamilika,” akasema Bw Komu.

Naye Mwenyekiti wa Shirika la Sauti ya Wanawake Lamu, Raya Famau, alisisitiza haja ya jinsia ya kike eneo la Pwani kupiganiwa kielimu na pia kinyadhifa mbalimbali serikalini ili nao pia wajivunie uhuru na maendeleo ya Kenya.

You can share this post!

Madaraka Dei 2021: Miaka 58 ya uhuru, Wakenya wana yapi ya...

Uhispania kuvaana na Ureno nao Uholanzi kukutana na...