Makala

Pwani yaanza mikakati ya kujiimarisha kiuchumi

November 1st, 2018 2 min read

Na SAMUEL BAYA

KAUNTI zote sita za Pwani zimeanza mikakati ya kujiimarisha kiuchumi.

Kaunti hizo kupitia kwa mwavuli wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani(JKP) zitaandaa kongamano la kilimo biashara, lengo kamili likiwa ni jinsi ya kufaidika na rasilmali zilizopo Pwani.

Kongamano hilo linalojulikana kama JABEIC litafanyika katika hoteli maarufu ya Ocean Beach iliyoko mjini Malindi.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, afisa mkuu wa JKP, Bw Emanuel Nzai alisema kuwa kongamano hilo litakuwa na mada ‘kubadilisha stori’ likimaanisha kubadilisha habari kuhusu kudorora kwa uchumi wa Pwani.

“Jambo muhimu katika kongamano hilo ni kuhakikisha kwamba kaunti zote sita zinakuja pamoja na kushirikiana kuboresha maendeleo. Ile habari ya kila siku kwamba tumedorora kimaendeleo inafaa kukoma,” akasema Bw Nzai.

“Kongamano hilo pia litatumika kama matayarisho ya kongamano kubwa la uchumi wa bahari ambalo litafanyika katika jiji la Nairobi mwezi ujao.

Kongamano hilo la linafanyika ili kuonyesha jinsi eneo la Pwani limejaaliwa kuwa na raslmali nyingi kama vile bahari na pia katika nyanja za kilimo na uwekezaji.

“Tuko na bahari na ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo. Tukitumia rasilmali hizi vizuri, ikiwemo madini, tunaweza kupiga hatua kubwa sana kimaisha na maendeleo kwa ujumla,” akasema Bw Nzai.

Aidha afisa huyo alisema tani 150,000 hadi 300,000 za samaki zinaweza kupatikana eneo hilo na hivyo kusaidia pakubwa kama kitega uchumi .

“Samaki zinaweza kuletea Pwani pato la kati ya Sh21 billioni na Sh42 billioni.Endapo lengo hili linaweza kufikiwa, basi tunaweza kuendeleza eneo hili kupitia kwa faida za uchumi unaotokana na bahari,” akasema Bw Nzai.

Awali juhudi za kujaribu kujikwamua kwa Pwani zilitatizwa na sababu mbalimbali ikiwemo kukithiri kwa umaskini na uhaba wa elimu, kutengwa kwa kimaeneo na hali duni ya usalama.

“Hata hivyo baada ya kuanzishwa kwa serikali za kaunti na JKP kuzinduliwa, kumekuwa na maendeleo kadha, ingawa sio mengi ambayo tunaweza kujivunia,” akasema afisa huyo.

Aidha kongamano hilo la Pwani litatekelezwa kupitia kwa awamu ya kwanza ya ustawi wa maendeleo eneo la Pwani ambayo imeorodheshwa katika kitengo cha uimarishaji wa chakula na usalama 2018-2030.

Ripoti hiyo ilitayarishwa na JKP pamoja na shirika la chakula ulimwenguni(FAO).

“Pia kongamano hili limelenga kutekeleza ajenda nne za Rais Uhuru Kenyatta ambazo baadhi yazo zimewekwa katika ustawi wa maendeleo ya taifa ya Ruwaza ya 2030. Baadhi ya ajenda hizo ni chakula cha kutosha na kuhakikisha kwamba hakuna Mkenya atakufa njaa kwa kukosa chakula,” akasema.

Eneo la Pwani kulingana na ripoti ya kiuchumi iliyotayarishwa na JKP, ina uwezo wa kuwa eneo kubwa la biashara kati ya 2015-2045.

“Ni soko kubwa la kibiashara ambalo linaweza kugeuza uchumi wa taifa hili. Eneo ambalo wawekezaji wanaweza kuja na kuwekeza,” sehemu ya ripoti hiyo ya JKP ilieleza.

Iliongeza, “Tuko na maeneo ya kuvutia ya kitalii pamoja na mbuga za wanyama za Tsavo. Tuna maeneo ambayo yanaweza kutumika kama viwanda. Ardhi ya kufanyia haya yote inapatikana Pwani.”

Serikali ya kitaifa imeanzisha mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa miradi mikuu na muhimu kwa maisha ya wakazi wa Pwani inatekelezwa.

Majuzi naibu Rais, Bw William Ruto alizindua ujenzi wa daraja ambao utagharimu Sh2.5 billioni katika eneo la Baricho, kaunti ya Kilifi. Miradi mingine inayotekelezwa ni pamoja na upanuaji wa bandari ya Mombasa na vile vile mpango wa kujenga bandari ya wazi katika eneo la Dongo Kundu.

Ni miradi hiyo ambayo Bw Nzai alisema ni muhimu kwa serikali za kaunti kuangalia jinsi ambavyo wataitumia kunufaika.

“JKP itatoa mwongozo kamili wa jinsi kaunti zote sita za Lamu, Kilifi, Kwale, Tana river, Mombasa na Taita Taveta zitatumia fursa ya miradi hii kumairisha maisha ya wakazi wa Pwani,” akasema.