HabariSiasa

Pwani yapangia Gavana Joho mikakati ya urais 2022

March 5th, 2018 2 min read

Na WANDERI KAMAU

Kwa ufupi:

  • Bw Joho ana cheo cha juu katika ODM, chama cha Wapwani kitamsaidia katika kujitetea kuhusu uwaniaji wa urais 2022
  • Huenda jamii ya Wapwani ikahisi kwamba nafasi yao imetimia, kwani uongozi wake katika serikali zilozopita umekuwa umegawanyika
  • Mazungumzo kuhusu kujitenga kwa Pwani yamekuwa yakisukumwa na haja ya kubuni chama huru cha kisiasa
  • Wadadisi wasema Joho anafaa aondoke katika ‘kivuli’ cha Bw Odinga na kujiimarisha kama mwanasiasa huru

HATUA ya viongozi wa ukanda wa Pwani kushinikiza kubuniwa kwa chama cha ukanda huo imetajwa kama mkakati wa kumpa nguvu Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuwania urais 2022.

Tayari, Gavana Amason Kingi wa Kilifi amesema mikakati ya kubuni chama hicho imeanza, ambapo wanashauriana na viongozi wengine wa kisiasa katika eneo hilo kuhakikisha wameafikia lengo hilo.

Wadadisi wanasema ingawa Bw Joho ana cheo cha juu katika ODM, chama cha Wapwani kitamsaidia katika kujitetea kuhusu uwaniaji wa urais kwenye uchaguzi ujao. Pia chama hicho cha Pwani kitampa fursa ya kuwa na mahala pa kukimbilia iwapo siasa za urithi wa Raila Odinga kama kiongozi wa ODM zitamzidia joto.

 

Kujaza pengo

Wachanganuzi wanasema kuwa Bw Joho yuko na nafasi bora kujijenga kisiasa na kufikia upeo wa kitaifa kutokana na pengo la kisiasa lililobuniwa na vinara wa NASA, Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) kutojitokeza Januari 30 wakati Raila Odinga alipokula kiapo cha “rais wa wananchi.”

Wadadisi wanadai kwamba kutojitokeza kwa watatu hao kulimpa Bw Joho nafasi kubwa kisiasa, ambayo huenda akatumia kutetea uwakilishi wa Pwani katika uchaguzi huo na jamii ya Kiislamu kwa jumla.

“Ilivyo kwa sasa, Bw Joho ndiye taswira kuu ya upinzani nchini. Amedhihirisha ujasiri usio wa kawaida, hasa katika kumtetea Bw Odinga. Ilivyo sasa, ndiye mrithi mkuu wa Bw Odinga ikiwa atang’atuka siasani,” asema Prof Herman Manyora, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana na Prof Manyora, sababu nyingine kuu ambayo huenda ikampa Bw Joho msukumo ni kutoka kwa jamii ya Kiislamu ambayo ingetaka kuwa na mmoja wao katika siasa za kitaifa.

Mchangazuzi mwingine, Maimuma Mwidau anasema kuwa huenda jamii hiyo ikahisi kwamba nafasi yao imetimia, kwani uongozi wake katika serikali zilozopita umekuwa umegawanyika.

 

Kuongeza usemi 

Wadadisi wa siasa za eneo la Pwani wanasema kwamba mazungumzo kuhusu kujitenga kwa eneo hilo yamekuwa yakisukumwa na haja ya kubuni chama huru cha kisiasa, ili kuongeza usemi wao katika ugavi wa nyadhifa kuu za kisiasa katika serikali ya kitaifa.

Anasema kuwa mustakabali wa Bw Joho katika ODM umeng’aa, ila anapaswa kuwa na “mpango mbadala” ikiwa kutazuka mafarakano katika urithi wa Bw Odinga.

Bali na hayo, asema kwamba sasa anafaa aondoke katika ‘kivuli’ cha Bw Odinga na kujiimarisha kama mwanasiasa huru.

Eneo la Pwani limekuwa likilalama kutengwa katika masuala muhimu ya kitaifa, huku baadhi wakishikilia kwamba imefikia wakati iwe na usemi mmoja katika siasa za kitaifa kwa ukombozi kamili wa kisiasa