Habari

Qatar kuongeza uwekezaji wake nchini Kenya

August 20th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

TAIFA la Qatar litawekeza katika sekta za kawi salama, makazi nafuu na mawasiliano nchini Kenya kama sehemu ya kuendeleza ushirikiano baina yake ya taifa hili.

Hayo ni kulingana na Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani ambaye Jumanne amtembelea Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Kwa upande wake Rais Kenyatta ameelezea kuridhika kwake na kuimarika kwa uhusiano kati ya Kenya na Qatar akisema taifa hili linakaribisha uwekezaji zaidi wa Qatar.

“Kama taifa rafiki tunashukuru serikali yene kwa kuendelea kuimarisha uchumi wetu kupitia uwekezaji na hata utalii. Na serikali yangu inachangamkia uwekezaji zaidi nyanja ya kawi salama, makazi nafuu na mawasiliano,” akasema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa taifa pia alitaja kuanzishwa kwa uchukuzi wa meli kati ya Mombasa na Doha pamoja na uzinduzi wa hivi majuzi wa ndege za moja kwa moja za Qatar hadi Mombasa mara mbili kwa wiki akisema kupitia kwayo ushirikiano kati ya raia wa mataifa haya mawili utaimarisha zaidi.

Abdulrahman Al-Thani, pia aliyewasilisha ujumbe kwa Rais Kenyatta kutoka kwa Mfalme wa Qatar Mstahiki Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, akisema taifa lake linathamini urafiki kati yake na Kenya na limekuwa makini katika kuunga mkono ukuaji wake kwa miaka mingi.

“Tunasalia kuwa mshirika imara wa Kenya katika nyanja zote. Tuko tayari hata kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuimarisha zaidi ushirikiano wetu,” akasema Abdulrahman Al-Thani

Naibu huyo wa Waziri Mkuu alikuwa ameandamana na Waziri wa Qatar wa Uchukuzi na Mawasiliano Jassim bin Saif Al Sulaiti na balozi wa Qatar hapa nchini Jabr Bin Ali Al Dosari.

Alimhakikishia Rais Kenyatta kwamba serikali yake itaunga mkono miradi inayoambatana na Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo akisema waekezaji kutoka Qatar wangependa kuekeza katika sekta ya nyumba.

Usalama wa kikanda

Kuhusu amani na usalama, Rais Kenyatta amemwarifu kiongozi huyo wa Qatar ufanisi ulioafikiwa kuimarisha usalama katika kanda hii ikiwemo Somalia na mkataba uliotiwa saini majuzi wa serikali ya mpito nchini Sudan.

“Bila amani, hutuwezi kuwa na maendeleo wala ustawi. Tunatumai kwamba nia iliyodhihirishwa katika kutia saini mkataba wa serikali ya mpito nchini Sudan itasaidia pakubwa kurejesha hali ya kawaida nchini humo,” Rais Kenyatta akamweleza kiongozi huyo wa Qatar.

Rais Kenyatta na mgeni wake pia wamejadili uwezekano wa kujumuisha lugha ya Kiarabu katika masomo kwenye Chuo cha Utalii ili kuwezesha vijana zaidi wa Kenya kujipatia ajira nchini Qatar.

Rais Kenyatta ameelezea matumaini yake kwamba kufuatia kufunguka kwa nyanja mpya za ushirikiano, kiwango cha biashara kati ya Kenya na Qatar kitaongezeka.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mshauri wa Ikulu, Nzioka Waita na mawaziri Monica Juma (Masuala ya Kigeni) na Fred Matiang’i (Waziri wa Ndani na Ushirikishi wa Serikali ya Kitaifa).