Makala

QUEEN NKIROTE: Sanaa iendelee kuvumishwa shuleni

June 2nd, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika kisanaa na kazi zake kutambulika kote duniani. Queen Nkirote Imanyara aachwi nyuma anaorodheshwa kati ya wasanii wanaolenga kujizolea umaarufu hapa nchini pia kufikia viwango vya waigizaji mahiri kimataifa kama Elizabeth Gillies mzawa wa Marekani na Lupita Nyong’o Mkenya anayetamba katika filamu za Hollywood.

Queen Nkirote Imanyara ni mwigizaji, ambaye kitaaluma amehitimu kama mwanahabari wa televisheni pia mfanyabiashara.

Mwigizaji huyu ambaye katika uhusika wake pia anajulikana kama Queen ni miongoni mwa wasanii ambao hushiriki kipindi cha ‘Tahidi High’ ambacho hurushwa kupitia Citizen TV kilicho kati ya vipindi maarufu hapa nchini.

”Tangu nikiwa mtoto nilitamani sana kuwa mwana habari pia mwigizaji ambapo licha ya kuhitimu kwa taaluma zote mbili, tasnia ya filamu imeyeyusha uahabari,” anasema na kudokeza kuwa amezamia kupalilia talanta yake kwa kuzingatia hakusomea masuala ya uigizaji.

Kisura huyu anasema anafanya uigizaji kama ajira maana hujitolea kufanya miondoko yake kadiri awezavyo wakati wowote anapopewa nafasi.

Demu huyu alianza kujituma katika masuala ya uigizaji mwaka 2012 ambapo alikuwa miongoni mwa wasanii walioshiriki kipindi cha ‘Vionja mahakamani’ kilichokuwa kinapeperushwa kupitia KBC Televisheni.

”Hata hivyo niliacha kazi katika kituo hicho na kuanza kazi kama ripota na shirika la GBS TV nilikofanya chini ya mwaka mmoja kabla ya kujiunga na Tahidi High mwaka 2014 hadi sasa,” alisema.

Anasema hapa nchini angependa kufanya kazi na wasanii kama Pascal Tikodi pia Catherine Kamau ambao wamefanya filamu ya ‘Selina’ na ‘Sue and Johnnie’ mtawalia.

Mwigizaji huyu anawataka maprodyuza wa tasnia ya maigizo nchini wawe wabunifu pia waengemee kuzalisha filamu zinazoendana na utamaduni wa taifa hili kama ilivyo katika mataifa yanayoendelea ikiwemo Nigeria na Afrika Kusini kati ya mengine.

Anatoa mfano wa filamu zilizotengezwa nao Philip Karanja na Abel Mutua waliofanya kazi tofauti sana na wengine lakini mwishowe iliibuka bora zaidi maana walifanya filamu zilizohusu maisha halisi humu nchini pia jinsi hali ilivyo mitaani.

”Kusema kweli hatua yetu waigizaji kutokumbatia utamaduni wetu imechangia wapenzi wa tasnia ya maigizo nchini kuvutiwa na filamu za kigeni hasa za Kinigeria (Nollywood),” alisema na kuongeza kwamba Wakenya wanastahili kuwa mstari wa kwanza kusapoti sanaa ya wazalendo kwa kununua pia kuhudhuria kumbi za kuonyesha filamu ili kutazama sanaa ya wenzao wanafavyofanya.

Pia anasema serikali inapaswa kuhakikisha kwamba somo la sanaa linaendelea kufunzwa shuleni maana wazazi wengi hawawezi kumudu karo kwa wanao kusomea katika mataifa ya nje.

Kadhalika anadokeza kuwa serikali inapaswa kukomesha mtindo wa kupiga marufuku baadhi ya filamu zinazozalishwa na wazalendo bali wawape nafasi kuonyesha talanta zao katika uigizaji.

Msichana huyu anayesema kuwa ndiyo wameanzisha familia na aliyekuwa mchumba wake siyo mchoyo wa mawaidha kwa waigizaji chipukizi. Anawahimiza kutovunjika moyo licha ya kukumbana na milima na mabonde katika ulingo huo.