Michezo

Quins hatimaye yaonja ushindi kwenye Ligi Kuu ya raga

November 23rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Harlequin hatimaye imevuna ushindi wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu ya raga nchini (Kenya Cup) baada ya kucharaza Menengai Oilers 25-15 uwanjani RFUEA jijini Nairobi, Jumamosi.

Wafalme wa zamani Quins walikuwa wameona vimulimuli pekee dhidi ya Homeboyz, KCB, Western Bulls na Nakuru kabla ya kupata ushindi huo muhimu unaotarajiwa kuwatoa mkiani kwenye ligi hii ya klabu 12.

Mabingwa watetezi KCB wametolewa kijasho chembamba kabla ya kunyamazisha “madeejay” Homeboyz 27-24 katika mechi ambayo wanabenki hao walilazimika kutoka nyuma 14-8 wakati wa mapumziko.

Washindi wa zamani Mwamba pia walikuwa na kibarua kigumu cha kutoka chini 7-3 wakati wa mapumziko katika uwanja wao wa nyumbani wa Nairobi Railways kabla ya kuzima Nondies 27-17.

Mabingwa wa mwaka 2016 Kabras Sugar walizidi kuandikisha ushindi mkubwa baada ya kukanyaga Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta 57-3 mjini Kakamega, huku mechi yake dhidi ya KCB ikinukia.

Matokeo (Novemba 23, 2019):

Kenya Harlequin 25-15 Menengai Oilers (RFUEA)

Western Bulls 10-23 Nakuru (Kakamega)

Kabras Sugar 57-3 Blak Blad (Kakamega)

Mwamba 27-17 Nondies (Nairobi Railways Club)

Kisumu 5-41 Impala Saracens (Kisumu)

KCB 27-24 Homeboyz (Ruaraka)