Habari Mseto

Rachel Ruto apigia debe mpango wa lishe shuleni


MAMA wa Taifa Rachel Ruto ameupigia debe mpango wa lishe shuleni, akiutaja kama unaosaidia watoto kutoka familia maskini nchini kupata masomo.

Akiongea katika Shule ya Msingi ya Mwatate katika Kaunti ya Taita Taveta wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika (Juni 16, 2024), Bi Ruto alisema kwa miaka mingi mpango huo umechangia idadi kubwa ya watoto kusalia katika shule za msingi na wengine kujiunga na shule za upili.

Mkewe Rais alieleza kuwa serikali imeonyesha kujitolea kwake kuimarisha masomo ya watoto kwa kuajiri walimu zaidi na kuanzisha masomo ya kompyuta shuleni.

“Serikali inachukua hatua za kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata elimu bora na katika mazingira faafu. Kupitia juhudi hizi za wadau wengine tunaweza kutimiza ndoto ya elimu kwa wote Barani Afrika,” Bi Ruto akasema.

Mama wa Taifa alisema serikali imepiga hatua kubwa katika kuendeleza haki na masilahi ya watoto.

Viongozi wa Kaunti ya Taita Taveta waliunga mkono kauli kuhusu umuhimu wa mpango wa utoaji lishe shuleni kwa wanafunzi.

Mbunge wa Mwatate, Peter Shake alisisitiza haja ya serikali kuingilia na kutatua changamoto zinazokumba watoto za ukosefu wa maji na lishe bora, haswa katika maeneo kame nchini.

“Tunahimiza serikali kuhakikisha kuwa mpango wa lishe shuleni unadumishwa ili kuwawezesha watoto kusalia shuleni kwa sababu wanakumbwa na changamoto nyingi nyumbani,” akasema.

Kwa upande wake Mbunge Mwakilishi wa Taita Taveta, Lydia Haika alishadidia umuhimu udumishaji wa mpango wa lishe shuleni na utatuzi wa shida ya ukosefu wa maji inayokumba wakazi na taasisi za masomo.

“Nyakati zingine watoto wetu hukosa kuhudhuria shule kwa sababu wao huenda kutafuta maji maeneo ya mbali. Katika hali hii, baadhi ya wasichana hubakwa wakiwa njiani kusaka maji. Tunaitaka serikali kuingilia kati na kusuluhisha tatizo hili la ukosefu wa maji,” akaeleza.

Kwa upande wake Gavana wa Taita Taveta, Andrew Mwadime pia aliongeza kuwa kaunti yake inakumbwa na tatizo la uhaba wa maji unaoathiri shughuli za masomo.

“Rais alikuwa ametuahidi kuwa utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa maji wa Mzima ungeanza. Pia tunahitaji shule zetu zisambaziwe matangi ya maji kuhakikisha kuwa watoto katika kaunti yetu wanapata maji na elimu wanayohitaji,” akaeleza.