Habari za Kitaifa

Rachel Ruto: Serikali itabuni kikosi kuombea polisi watakaotumwa Hati

March 24th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MKEWE Rais William Ruto, Bi Rachel Ruto, ametangaza kwamba serikali itabuni kikosi maalum cha maombi, kwa lengo la kuombea polisi watakaotumwa na serikali kwenda kudumisha amani nchini Haiti.

Bi Ruto alitoa tangazo hilo mnamo Jumamosi, Machi 23, 2024, wakati wa uzinduzi wa albamu ya muziki ya ‘Fourth Man’ na kundi la 1005 Songs & More katika hoteli moja jijini Nairobi.

Alisema kuna hitaji kubwa la uwepo wa maombi, “kwani serikai haiwezi kuwaruhusu polisi hao kwenda nchini Haiti bila kuombewa”.

“Tumekuja pamoja kusema tunataka kubuni mkakati wa maombi, na tungependa muungane nasi katika kuliombea taifa hilo la Haiti, kwani tunaamini Mungu anaweza akalibadilisha. Tumeona kile Mungu ameifanyia nchi ya Kenya. Tunaamini kwamba Mungu anaweza akayafanyia hivyo mataifa tofauti kote duniani,” akaongeza.

“Hatuwezi kuruhusu polis wetu kwenda nchini Haiti bila maombi. Tulikuwa na mapasta kutoka Haiti na Amerika; na tunajaribu kuona vile mataifa hayo matatu yanaweza kuungana ili kuomba pamoja. Tunaamini kwamba kila kitu kinawezekana kupitia maombi,” akaeleza.

Bi Ruto alisema amekuwa kwenye mkutano wa siku mbili kujadili kuhusu suala hilo.

Mkutano huo uliwashirikisha mapasta kutoka Haiti na Amerika.

Hilo linajiri baada ya Rais William Ruto kutangaza mpango wa kupeleka kikosi cha polisi kutoka Kenya, kuvisaidia vikosi vya taifa hilo kudumisha amani dhidi ya magenge ya uhalifu ambayo yamekuwa yakiendeleza vitendo vya kikatili.

Hata hivyo, Rais Ruto alisema atafanya hivyo baada ya taifa hilo kupata serikali rasmi.