Michezo

Rachier afichua Makwatta amemuomba msamaha

September 4th, 2019 1 min read

Na CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa Gor Mahia Ambrose Rachier amefichua kwamba mwanasoka John Mark Makwatta amemwomba radhi baada ya kujiunga na AFC Leopards siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho wa wanasoka Jumatatu.

Akizungumza na Taifa Leo, Rachier alisikitikia kusambazwa katika majukwaa ya mitandao ya kijamii kwa hundi ya Sh1 milioni yenye saini yake ambayo alitoa kwa mwanasoka huyo kama ada ya uhamisho ili ajiunge na K’Ogalo kabla ya Makwatta kugeuka na kujiunga na AFC Leopards.

“Makwatta aliwasili katika afisi yangu saa 10 jioni pamoja na ajenti wake akisema kwamba anataka kuchezea Gor Mahia. Nilizungumza na meneja wetu wa timu ambaye alitayarisha stakabadhi zote na nikatia saini sehemu yangu,” akasema Rachier.

Kulingana naye alilazimika kutia saini hundi hiyo baada ya Makwatta kutaka pesa taslimu na wakati huo hawangeweza kupata fedha hizo kwa kuwa benki tayari zilikuwa zimefungwa.

“Kabla hatujakamilisha mchakato wa usajili, Makwatta alishikilia kwamba alitaka pesa taslimu na wakati huo pesa hizo hazingepatikana kwa kuwa benki zilikuwa zimefungwa. Tulikubaliana kisha nikatia saini hundi ya Sh1 milioni na nikamkabidhi. Gafla bin vuu aliomba kuenda haja baada ya kuchukua hundi na tuliyosikia baadaye ni kwamba amejiunga na AFC Leopards,’’ akaongeza Rachier.

“Ameniomba radhi lakini wanasoka nchini wanafaa kufanya mambo yao kiheshima ili kuzuia matukio kama hayo,” akaendelea.

Mwenyekiti wa AFC Leopards, Dan Shikanda naye alisema hakufahamu kwamba Gor Mahia walimkabidhi Makwatta hundi hiyo, akisisitiza wamekuwa wakishauriana naye kwa lengo la kupata huduma zake.

“Nilimsubiri siku yote Jumatano baada ya kuniambia alikuwa akielekea kusikiza ofa ya Gor Mahia na Wazito. Alisaini mkataba nasi saa nne usiku baada ya kuridhika na ofa yetu. Hata hivyo ni vibaya kama alichukua hundi ya Gor na hata kusambaza picha yake kwenye mitandao ya kijamii.”