Radi yaua 60 wakiwemo 11 waliokuwa wakipiga ‘selfie’

Na MASHIRIKA

NEW DELHI, India

WATU 60, wakiwemo 11 waliokuwa wakipiga picha za ‘selfie’ kwenye mvua, walifariki baada ya kupigwa na radi katika wilaya 16 nchini India.

Watu 20 walijeruhiwa vibaya huku mifugo 250 wakiuawa katika mkasa huo.

Miongoni mwa waliouawa kwenye mkasa huo uliotokea Jumapili, 14 walikuwa wakazi wa wilaya ya Prayagraj, jimbo la Uttar Pradesh.

Waziri Mkuu Narendra Modi alisema kuwa, kila familia iliyopoteza jamaa itapewa Sh185,300 za kufutia machozi. Waliojeruhiwa watalipwa fidia ya Sh46,300 na waliopoteza mifugo na mazao yao pia watalipwa fidia. Serikali za majimbo pia zimetangaza kutoa msaada wa kifedha kwa waathiriwa.

Wengi wa waliokufa walikuwa watoto na wanawake.

Jumamosi, watu wengine 20 waliuawa na radi katika majimbo ya Uttar Pradesh na Rajasthan.

Afisa Mkuu wa Polisi Anand Srivastava alisema miongoni mwa waliokufa, 11 walikuwa wakipiga picha za selfie katika mnara wa kitaifa wa Amber Fort mjini Jaipur, kabla ya kupigwa na radi, Jumapili. Watu sita walipigwa na radi katika eneo la Soraon na wawili waliangamia kijijini Koraon.

Maeneo mengine yaliyoshuhudia vifo kwenye mkasa huo wa radi ni Prayagraj na Firozabad.

Wakulima wawili waliuawa na radi walipokuwa wakifanya kazi kwenye mashamba yao katika eneo la Ramsevak. Mvua ilipoanza kunyesha, wawili hao, walienda kujikinga chini ya mti kabla ya radi kutokea na kuwaua papo hapo.

Mwanamume mmoja alifanikiwa kuokoa familia yake kwa kuwakimbiza watoto wake ndani ya nyumba na radi ilipotokea iliua mifugo wake 42.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa watu 2,876 na 2,357 walifariki kwa kupigwa na radi nchini India mnamo 2019 na 2018 mtawalia.

Visa vya watu kuuawa kwa radi nchini India huwa vingi kati ya Juni na Septemba kila mwaka ambao ni msimu wa upepo mkali unaovuma kutoka baharini na huandamana na mvua.

Mnamo 2019, watu 400 waliuawa kwa radi jimboni Bihar (400), Madhya Pradesh (400), Jharkhand (334) ana Uttar Pradesh (321).

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya India (NWS) iliwashauri raia wa nchi hiyo kuhakikisha kuwa wanaingia ndani ya nyumba mvua inapoanza kunyesha.

Idara hiyo ilisema kuwa, japo radi haina kinga, kuingia ndani ya nyumba kunaweza kusaidia pakubwa kupunguza vifo.

“Mvua inapoanza kunyesha, ingia ndani ya nyumba. Nyumba zilizojengwa kwa mawe au matofali zinazuia makali ya radi. Ukiwa ndani ya gari, hakikisha kuwa unafunga mlango na madirisha,” ikashauri idara ya NWS.