Habari MsetoSiasa

Rafiki asimulia siku Moi alihofiwa kufariki ajalini

February 10th, 2020 1 min read

 WYCLIFF KIPSANG na FLORAH KOECH

RAIS Mstaafu Daniel Arap Moi alihusika katika ajali alipokuwa akielekea Nairobi mara ya kwanza kutekeleza majukumu yake kama mbunge, mmoja wa marafiki zake wa zamani amefichua.

Mzee Harun Bomett ambaye ni binamu ya mkewe Moi, marehemu Lena Moi, jana alieleza vile walikutana na Moi mjini Kabarnet mnamo 1957 walipokuwa wakisafirisha mbao kupeleka Nairobi. Alisema Moi alikuwa amekwama mjini humo baada ya kukosa usafiri.

“Alikuwa ameanza kazi yake katika bunge (Legco) na hakuwa amenunua gari. Aliomba tumpe lifti,” Bw Bomett aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano nyumbani kwake eneo la Kaploo, kaunti ndogo ya Eldama Ravine.

“Alikubali kuketi nyuma, juu ya mbao kwa sababu sehemu ya mbele ya lori ilikuwa imejaa. Tulipofika Timboywo, tulisimama kunywa chai katika mkahawa wake ambao ulikuwa ukisimamiwa na Lena kabla ya kuendelea na safari,” akaongeza Mzee Bomet mwenye umri wa miaka 83.

Hata hivyo, lori hilo liliharibika kila mara barabarani na wakati mmoja lilikosa mwelekeo na kuanguka baada ya kugonga mti. Lakini walinusurika.

Mzee Bomet alisema baada ya ajali hiyo waliamua kutembea kwa miguu huku Moi akitaraji kuwa msamaria mwema angewasaidia kwa sababu hakutaka kukosa kuhudhuria bunge jijini Nairobi.

Bila wao kufahamu, habari zilikuwa zimeenea kwamba walihusika katika ajali mbaya na wote wakafa.

“Baada ya kutembee kwa zaidi ya kilomita 30, tuliamua kuoga katika mto Kimng’orom kwa sababu tulikuwa wachovu mno. Lakini baada ya muda mfupi tulisikia lori likikaribia. Ilitulazimu kuvalia nguo haraka na kuelekea huku upande ambako sauti ya lori ilisikika,” Bomet anakumbuka.

“Watu waliokuwa kwenye lori hilo walidhani tulikuwa mizimwi kwa sababu walikuwa wamejulishwa kwamba tulifariki baada ya kupata ajali. Hata hivyo, walikubali kutubeba,” akaongeza.