Raga: Kabras, Oilers juu ligi ikienda Krisi

Raga: Kabras, Oilers juu ligi ikienda Krisi

GEOFFREY ANENE na TITUS MAERO

WANASUKARI wa Kabras Sugar na Menengai Oilers walifunga mwaka katika nafasi mbili za kwanza kwa alama 20 baada ya kuzoa ushindi wao wa nne mfululizo kwenye Ligi Kuu (Kenya Cup) mnamo Jumamosi.

Viongozi Kabras walikung’uta wenyeji Impala Saracens 24-12 kupitia miguso ya Derrick Ashiundu (miwili), Hillary Mwanjilwa na Ephraim Oduor na mikwaju ya Ntabeni Dukisa ugani Impala jijini Nairobi. Impala, ambayo bado haina pointi baada ya kujibwaga uwanjani mara nne mfululizo, ilifunga penalti kupitia kwa Quinto Ongo (tatu) na Martin Juma.

Oilers imeng’oa mabingwa watetezi KCB kutoka nafasi ya pili baada ya kuzamisha Masinde Muliro (MMUST) 30-19 kupitia kwa miguso ya Clinton Odhiambo, Tyson Maina, Davis Nyaundi na Geoffrey Ominde. Vijana wa kocha Gibson Weru pia waliona lango kupitia kwa Timothy Omela aliyeongeza penalti mbili na idadi sawa ya mikwaju.

Wenyeji Mmust, ambao wakati mmoja walikuwa chini 22-0, walipata alama zao kupitia kwa Erick Cantona (penalti tatu na mkwaju) na Claus Shirievo (mguso) mjini Kakamega. “Ushindi mtamu tuliostahili alama tano. Vijana walicheza vyema.

Tulifanya kazi nzuri sana katika idara zote na ninafurahi jinsi tulivyocheza,” Weru alisema katika mahojiano baada ya mechi. Wiki hiyo ya nne ya ligi hiyo ya klabu 12 zilishuhudia Homeboyz na Nondescripts zikivuna ushindi wa kwanza wa msimu.

Zote zilikuwa zimepoteza michuano mitatu ya kwanza. ‘Madeejay’ wa Homeboyz walinyamazisha wenyeji wao Kenya Harlequin 23-12 ugani RFUEA nao washikilizi wa rekodi ya mataji mengi Nondescripts wakapiga breki Strathmore Leos 22-15 uwanjani Ngong Racecourse.

Mabingwa wa zamani Top Fry Nakuru pia walitia kapuni alama za kwanza za msimu baada ya kutoka 10-10 dhidi ya Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ugani Nakuru Athletic. Mechi kati ya Mwamba na mabingwa watetezi KCB iliyoratibiwa kuwa ya kwanza uwanjani Impala, iliahirishwa baada ya visa vya virusi vya corona kushuhudiwa kambini mwa Mwamba.

Ligi imeingia mapumzikoni hadi Januari 8. Jedwali: Kabras Sugar (alama 20), Menengai Oilers (20), Strathmore Leos (16), Kenya Harlequin (13), KCB (tisa), Mmust (tisa), Blak Blad (saba), Homeboyz (tano), Nondies (tano), Nakuru (mbili), Mwamba (moja), Impala Saracens (sifuri).

You can share this post!

Jasiri wa Kenya watamba miereka ya Tong-Il Moo-Do

Maaskofu wahimiza serikali ikarabati daraja la mto Enziu

T L