Michezo

RAGA YA DUNIA U-20: Chipu yatafunwa na Uruguay kama njugu karanga

July 11th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 ya Kenya almaarufu Chipu, ilikaribishwa katika Raga ya Dunia kwa kichapo kikali cha alama 63-11 mjini Sao Paulo nchini Brazil, Julai 9 usiku.

Alama za Kenya katika mchuano huu wa Kundi A zilipatikana kupitia kwa mguso wa nguvu-mpya Samuel Were naye nahodha msaidizi Dominic Coulson akachangia penalti mbili.

Uruguay ilitangaza hali ya hatari mapema ilipochukua uongozi wa 7-0 baada ya Sonneveld Malleret kupachika mguso uliondamana na mkwaju kutoka kwa D’Avanzo Ferres katika dakika ya kwanza.

Kenya ilijipata chini 14-0 baada ya Rippe Welker na Ferres kuongeza mguso na mkwaju dakika ya tano, mtawalia.

Penalti ya Coulson dakika nne baadaye ilipunguza uongozi wa Uruguay hadi 14-3, lakini ilikuwa sawa na kuchokoza nyuki kwenye mzinga kwa sababu ilijipata chini 39-3 wakati wa mapumziko baada ya kufungwa miguso mitatu bila jibu kutoka kwa Amaya, Cat de Posadas na Etchegorry Pugh, miwili ikiandamana na mikwaju kutoka kwa Ferres, ambaye pia aliongeza penalti mbili.

Kenya ilifanya badiliko mapema katika kipindi cha pili kwa kuingiza Ian Masheti katika nafasi ya Rotuk Rahedi, lakini hili halikuzuia Uruguay kuongeza mwanya hadi 51-3 kupitia miguso ya Acros Perez Picardo na Garese Pastorino iliyoandamana na mkwaju mmoja kutoka kwa Ferres. Coulson alipunguza pengo hilo hadi 51-6, lakini tena ikakubali mguso bila mkwaju kutoka kwa Welker.

Were aliingia uwanjani dakika ya 55 katika nafasi ya James Mcgreevy naye George Kiryazi akajaza nafasi ya Sheldon Kahi sekunde chache baadaye, huku Uruguay pia ikifanya mabadiliko matatu kabla ya alama zaidi kushuhudiwa katika mchuano huu.

Mguso kutoka kwa Malleret ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Ferres katika dakika ya 60 ulifuatwa sekunde chache baadaye na mguso wa pekee wa Kenya kutoka kwa Were. Coulson alikosa mkwaju wake.

Hakuna alama zaidi zilifungwa tena, ingawa Kenya iliwapa wachezaji Owain Ashley na Barry Young dakika za kujionyesha uwanjani walipojaza nafasi za Michele Brighetti na nahodha msaidizi Samuel Asati katika dakika 12 za mwisho.

Wachezaji wa Chipu walijaribu binafsi kusumbua Uruguay, lakini walinzi wa Uruguay walikuwa macho kuzuia kufungwa alama zaidi.

Marekebisho

Katika mahojiano baada ya mechi, Kocha Mkuu wa Kenya, Paul Odera alikiri kuna idara nyingi zinazohitaji kurekebishwa kabla ya mechi ijayo dhidi ya wenyeji Brazil zikiwemo ikabu, mbinu za makabiliano na kujiamini.

Aliongeza, “Sisi hutafuta kumaliza mechi kwa nguvu katika kipindi cha pili na hiyo iliyonekana katika mchuano huu. Cha muhimu ni wachezaji kujifunza kutokana na mechi za kiwango hiki.”

Washindi wa mwaka 2008 Uruguay wanaongoza Kundi A kwa alama tano, sawa na mabingwa wa mwaka 2014 na 2017 Japan, ambao walikanyaga Brazil 56-24. Kenya, ambao waliandaa makala ya mwaka 2009 na kumaliza katika nafasi ya nne, na washiriki wapya kabisa Brazil hawana alama.

Washindi wa medali ya fedha mwaka 2017 na shaba mwaka 2018 Ureno wanaongoza Kundi B kwa alama tano baada ya kupepeta Hong Kong 59-27.

Nambari mbili Tonga, ambao walimaliza mwaka 2012 katika nafasi ya tatu na 2014 katika nafasi ya pili, pia wamezoa alama tano baada ya kulima washindi wa medali ya fedha mwaka 2013 na 2015 Canada japo pembamba 26-25.

Canada inashikilia nafasi ya tatu kwa alama mbili nayo Hong Kong inavuta mkia bila alama. Mashindano haya yatakamilika Julai 21.