Michezo

Raha Kenya kutwaa ubingwa wa Riadha za Afrika

August 7th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wapya wa Riadha za Afrika, Kenya wanatarajiwa walirejea nyumbani Jumatatu  kutoka nchini Nigeria walikojizolea medali 11 za dhahabu, fedha sita na shaba mbili mjini Asaba kati ya Agosti 1-5, 2018.

Kenya iliingia siku ya mwisho ya riadha hizi za watu wazima ikishikilia nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa watetezi Afrika Kusini na mabingwa wa zamani Nigeria.

Hata hivyo, ilijikakamua na kuonyesha weledi wake wa kuchana mbuga na kujiongezea nishani sita za dhahabu kupitia kwa Edward Zakayo (mita 5,000), Beatrice Chepkoech (mita 3,000 kuruka viunzi na maji), Elijah Manangoi (mita 1,500), Samuel Gathimba (matembezi ya kilomita 20), Julius Yego (kurusha mkuki) na timu ya mbio za mita 4×400 kupokezana vijiti ya wanaume (Alphas Kishoyian, Aron Koech, Emmanuel Korir na Jared Momanyi) na kurejesha taji ililokuwa imeshinda mara ya mwisho mwaka 2010 jijini Nairobi.

Wanariadha wengine walioshindia Kenya medali za dhahabu ni Hellen Obiri (mita 5,000), ambaye alikuwa Mkenya wa kwanza kushinda medali mjini Asaba, Conseslus Kipruto (mita 3,000 kuruka viunzi na maji), Mathew Sawe (kuruka juu), Winny Chebet (mita 1,500) na Stacy Ndiwa (mita 10,000). Emmanuel Korir (mita 800), Alice Aprot (mita 10, 000), Chespol (mita 3,000 kuruka viunzi na maji), Grace Wanjiru (matembezi ya kilomita 20), Timothy Cheruiyot (mita 1,500) na timu ya mbio za mita 4×400 kupokezana vijiti ya wanawake, walishinda nishani za fedha.

Timu ya mbio za mita 4×100 ya kupokezana vijiti ya wanawake (Eunice Kadogo, Millicent Ndoro, Joan Cherono na Freshia Mwangi) pamoja na Fancy Chemutai (mita 3,000 kuruka viunzi na maji) waliletea Kenya medali za shaba. Kenya iliwakilishwa na wanariadha 64 katika makala haya ya 21 yaliyovutia mataifa 52.

Jedwali la Riadha za Afrika (2018):

Taifa Dhahabu  Fedha  Shaba  Jumla

Kenya        11     6       2       19

Afrika Kusini       9       13     8       30

Nigeria       9       5       5       19

Morocco    2       5       4       9

Ethiopia     2       3       4       8

Tunisia       2       2       4       8

Ivory Coast         2       2       2       6