Habari Mseto

Raha kwa wenye mikokoteni na punda bodaboda kupigwa marufuku

August 29th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAENDESHAJI mikokoteni na wamiliki wa punda kwenye miji ya kale ya Lamu na Shella wamepata afueni kufuatia hatua ya hivi majuzi ya serikali ya kaunti hiyo ya kupiga marufuku uendeshaji pikipiki, baiskeli na magari ndani ya miji hiyo ya kihistoria.

Mara nyingi wamiliki wa punda na waendehsaji mikokoteni eneo hilo wamejitokeza kulalamikia ongezeko la wahudumu wa boda boda ndani ya miji ya Lamu na Shella, jambo ambalo linawanyima biashara.

Baadhi ya waendeshaji mikokoteni na wenye punda wamelazimika kuacha biashara hiyo kutokana na ukosefu wa wateja.

Waliozungumza na Taifa Leo Jumatano aidha waliipongeza serikali ya kaunti ya Lamu kwa hatua yake ya kupiga marufuku boda boda ndani ya mji wa Lamu.

Watalii wafurahia huduma za punda mjini Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Walisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kurejesha upya hadhi ya biashara ya waendeshaji mikokoteni na wenye punda ambao walikuwa tayari wamefungiwa nje ya biashara hiyo ya tangu jadi.

Msemaji wa waendeshaji mikokoteni eneo la Lamu Omar Kidege alisema tangu kupigwa marufuku kwa wahudumu wa boda boda kutekeleza shughuli zao ndani ya miji ya Lamu na Shella, wenye mikokoteni na punda wamekuwa wakivuna pakubwa kutokana na ongezeko la wateja.

Anasema kabla ya marufuku hiyo kuamriwa, wateja wengi na mizigo yao walikuwa wakikimbilia kubebwa na boda boda.

Bw Mohamed Omar akiwa juu ya punda wake. Picha/ Kalume Kazungu

“Tunashukuru kwamba biashara ya usafiri kwa kutumia mikokoteni na punda imeanza kufufuka. Boda boda walikuwa wametuharibia biashara.

Wateja walikuwa wakikimbilia kusafirishwa kwa pikipiki kwa sababu ya uharaka wake. Hatukuwa na soko. Tunapongeza kaunti kwa kupiga marufuku pikipiki ndani ya kisiwa cha Lamu na Shella. Angalau biashara yetu imenoga sasa,” akasema Bw Kidege.

Kauli yake pia iliungwa mkono na Bw Ahmed Yusuf ambaye ni mwendeshaji punda maarufu kisiwani Lamu aliyesema wasafiri hawana budi ila kutafuta huduma zao kila wanapowasili na mizigo kisiwani Lamu.

Waendeshaji mikokoteni wakitekeleza shughuli zao kisiwani Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Yusuf aliiomba kaunti kutilia mkazo sheria hiyo ili kuhifadhi hadhi na ukale wa mji wa Lamu.

“Sisi tumezoe usafiri wa punda, mikokoteni na miguu. Haya mambo ya kisasa yanaharibu hadhi ya mji wetu. Tumefurahia sana sheria mpya ya kukataza pikipiki ndani ya mji. Tuendelee kutumia punda, mikokoteni na miguu kuhifadhi utamaduni na historia ya miji yetu,” akasema Bw Yusuf.

Mnamo 2001, mji wa kale wa Lamu uliorodheshwa na Shirika la Kisayansi, Elimu na Utamaduni ulimwenguni (UNESCO) kama eneo mojawapo linalotambulika zaidi kwa kuhifadhi tamaduni na ukale wake, yaani-UNESCO World Heritage Site.