Michezo

Raha mitandaoni baada ya Mourinho kutimuliwa

December 18th, 2018 2 min read

NA CECIL ODONGO

MASHABIKI kote duniani walimiminika katika mitandao ya kijamii kusifu usimamizi wa Manchester United baada ya kumpiga kalamu kocha Jose Mourinho Jumanne kufuatia msururu wa matokeo duni tangu msimu wa 2018/19 uanze.

“Manchester United inatangaza kwamba kocha Jose Mourinho ametimuliwa kutoka wadhifa wake mara moja. Klabu inamshukuru Jose kwa huduma alizotoa kipindi chote akiwa Manchester United na kumtakia kila la kheri katika kazi yake ya ukocha.”

“Kaimu kocha atateuliwa kusimamia timu hadi mwisho wa msimu huu huku klabu ikizamia mchakato kabambe wa kumtafuta kocha mpya wa kudumu msimu ujao wa 2019/2020,” ikasema taarifa ya kutimuliwa kwa Mourinho.

Mashabiki wa timu hiyo walizamia mtandao wa kijamii wa Twitter kusifu kufutwa kwa Mourinho.

“Ahsanteni Man U kwa kuboresha mwaka wangu kutokana na kumfuta kocha huyo. Mwaka wangu ulikuwa mbaya ila sasa umebadilika baada ya kupokea taarifa hii,” akasema@NL7 Renderza.

@Kenkatee naye alisema “ Man U mlishinda mechi moja Septemba, Oktoba na Novemba mtawalia. Ilikuwa kama nyakati za kupitia hedhi na hamngeshinda Disemba mngekuwa wajawazito,”

“Ni wazi kwamba Mourinho ni mtaalamu wa kukosa ufanisi baada ya kila miaka mitatu. Hata hivyo nafurahi jinsi ulivyofanyakazi mwaka wa kwanza. Bado wewe ni spesheli,” akasema @Benjaminaisya.

Wengine walitumia picha za wachezaji hasimu na maadui wa Mourinho kama Pogba, Valencia, Fellaini na Sanchez kumkejeli mkufunzi huyo.

Manchester United maarufu kama Red Devils kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL. Wamepoteza mechi tano kati ya 17 walizoshiriki huku tofauti ya alama 19 ikitamalaki kati yao na viongozi Liverpool.

Vile vile mwanya wa alama 11 inawatenganisha na nambari nne Chelsea wakati klabu mbalimbali kubwa zinaendelea kupigania nafasi ya kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Barani msimu ujao wa 2019/20.

Mourinho amehudumu klabuni humo kwa muda wa miaka miwili na inakisiwa kichapo cha 3-1 Man U kililishwa na viongozi Liverpool Jumapili Disemba 16 kilichochea kutimuliwa kwake.

Baada ya kichapo alinukuliwa akisema timu hiyo imesalimu amri kwenye mbio za kufukuzia ubingwa wa EPL na pia amekuwa kwenye uhusiano baridi na wanasoka wa timu hiyo kama Alexis Sanchez, Anthony Martial na Paul Pogba.