Habari Mseto

Raha mitandaoni mwanamume kutoweka na hongo ya polisi Embu

February 20th, 2020 1 min read

NA ELVIS ONDIEKI

MWANAMUME katika Kaunti ya Embu, aliwaacha polisi wa trafiki vinywa wazi baada ya kutoweka na mabunda ya noti waliyokuwa yamekusanya kama hongo kutoka kwa wahudumu wa matatu.

Kisa hicho ambacho kimesifiwa na Wakenya mitandaoni kama funzo kwa polisi wafisadi, kilitokea katika kituo cha biashara cha Kathageri kwenye barabara kuu ya Nairobi – Meru.

Dereva aliyeshuhudia sakata hiyo aliambia Taifa Leo jinsi mwanaume huyo alivyojitokeza kutoka kichakani na kuchukua noti hizo ambazo zilikuwa ndani ya mkoba uliokuwa umefichwa kwenye majani kando ya barabara.

Baada ya kuzichukua aliwapiga chenga maafisa hao na kutorekea kichakani mbio mbio.

Dereva huyo ambaye alikuwa akiendesha gari karibu na mahala pa tukio hilo, alisema kulikuwa na maafisa wawili wa trafiki, mmoja wa kiume na mwingine wa kike.

Afisa wa kiume alijaribu kumkimbiza mwanaume huyo bila mafanikio na alilazimika kukata tamaa na kuanza kurusha matusi akimlaani mwanaume huyo kwa kutoweka na ‘jasho’ lao.

“Kuna sehemu ya miinuko ambayo inaunganisha barabara hii na hapo ndipo mwanaume huyo alipitia kwa kasi ya ajabu na kuwazidi polisi hao mbio. Alipogundua kwamba hangemfikia, afisa wa kiume alimpigia kelele akimwagiza asimame lakini aliongeza mwendo na kuyoyomea kwenye kichaka,” akasema shahidi huyo.

Nafuu kwa mwanaume huyo ni kwamba polisi hao hawakuwa wamejihami kwa bunduki, bali walikuwa wamebeba tu bakora zao za kawaida.

Wakati wa kisa hicho wahudumu wa matatu na wasafiri walikuwa wakishangilia mwizi huyo akitoweka na kufurahia kwa kuwaibia polisi ambao huwa wanahangaisha wasafiri wakiitisha hongo.

Kutokana na oparesheni kali za makachero wa Tume ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi (EACC), polisi wa trafiki wanaochukua hongo huwa hawaweki rushwa hiyo mfukoni kama zamani bali huficha fedha hizo kwenye mkoba unaowekwa mahali fiche karibu na barabara.

Kwenye maeneo ambayo kazi ya kuelekeza magari huwa ni nyingi, polisi hutumia raia kuchukua fedha hizo kwa niaba yao kisha wanamgawia baada ya kumaliza shughuli.