Michezo

Raha tele kwa kocha timu yake kuangusha Mathare

July 31st, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI  wa Klabu ya SoNy Sugar Patrick Odhiambo hakuweza kuficha furaha ribo ribo zilizomjaa baada ya wanasukari hao kuvuna ushindi wa  2-0 dhidi Mathare United Julai 29 katika mechi ya KPL iliyosakatwa ugani Awendo, Kaunti ya Migori.

Ushindi huo ulihakikisha Mathare United inayonolewa na kocha msifika Francis Kimanzi inahitimisha mechi za mwezi Julai bila kuandikisha ushindi wowote na kuendeleza mtindo wa kusajili matokeo mabaya.

Huku akimminia sifa kocho kocho mfungaji wa mabao hayo mawili Tobias Otieno, kocha huyo alisema matokeo hayo yamewapunguzia presha zilizowakumba za kuhofia kuteremshwa ngazi mwisho wa msimu.

Aidha alifichua kwamba kabla mtanange huo aliwapa wanasoka wake maagizo yaliyowaongoza kukabili  Mathare United na kwa kweli wachezaji hao waliyafuata maagizo hayo ndiposa wakaibuka na ushindi huo.

“Mathare United inajulikana kwa usakataji kabumbu wa kuavamia lango la wapinzani. Niliwashauri wachezaji wangu wasibane wala wasivamie bali waingie mchezoni na kujiburudisha kwa soka tamu ili kuwasahaulisha mtindo wa uchezaji tukilenga mipira mingi langoni mwao,” akafichua mkufunzi huyo.

“Bado tupo vitani kwa kuwa tunalenga kusajili matokeo yatakayotuepushia hatari ya kushushwa daraja mwisho wa msimu tukiwa tumesalia na mechi 10,” akaongeza Odhiambo.

Ushindi huo uliwapaisha SoNy  hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 27, pointi nne nje ya mduara unaozingira timu ambazo huenda zikashushwa ngazi.