NA KNA
SEKTA ya Utalii (KTB) imejawa na furaha baada ya meli iliyo na watalii 620 kutia nanga katika bandari ya Mombasa.
Akiwapokea wageni hao, Katibu wa Wizara ya Utalii John Ololtua alisema kufika kwa meli hiyo kwa jina World Odyssey ni ishara sekta ya utalii imeanza kunoga.
Bw Ololtua aliandamana na maafisa wakuu katika Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) na wakuu wa bodi ya utalii nchini (KTB) kuwalaki watalii hao.
Katibu huyo alisema watalii wameanza kuwa na imani na nchi hii.
Alisema sekta ya utalii imeanza kupata umaarufu tena nchini na pia katika lingo za kimataifa.
Meli hiyo kwa jina World Odyssey iko na watalii 620 na wahudumu 175.
Meli hiyo Ilifika katika bandari ya Mombasa kutoka Mumbai, India na inatarajiwa kukaa kwa siku sita kabla ya kuenda nchini Jordan.
Bw Ololtua alisema wengi wa watalii hao ni wanafunzi wa vyuo vikuu watakaokaa nchini kubadilishana mawazo na wanafunzi wa vyuo humu nchini.
“Niko na uhakika baadhi ya wageni hawa watapata fursa ya kutembelea hifadhi za mbuga za wanyama wa pori. Jambo hili litapiga jeki sekta ya utalii, ”alisema Bw Ololtua.