HabariSiasa

Rais alaumiwa kuyumbisha nchi

July 1st, 2019 2 min read

Na BERNADINE MUTANU

IDADI kubwa ya Wakenya wanamlaumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kupeleka nchi mkondo mbaya, utafiti umeonyesha.

Kulingana na utafiti uliofanywa na shirika la Infotrak, asilimia 26 ya Wakenya wanasema Rais Kenyatta ndiye wa kulaumiwa kwa matatizo yaliyopo nchini hasa gharama ya juu ya maisha, ukosefu wa ajira na ufisadi.

Asilimia 15 ya raia nao wanawalaumu wanasiasa kwa jumla kwa matatizo haya, Naibu Rais William Ruto (asilimia tatu) na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga (asilimia moja).

Kulingana na matokeo ya utafiti huo yaliyotangazwa jana, Wakenya wengi (asilimia 48) wanaamini nchi imechukua mwelekeo mbaya hasa kutokana na ukosefu wa ajira, gharama ya juu ya maisha na ufisadi. Katika mikoa yote masuala haya matatu yalitajwa kama matatizo makuu yanayolikumba taifa.

Mkoa wa Magharibi unaongoza kwa idadi kubwa ya watu wanaohisi nchi inaelekea vibaya kwa asilimia 57 ukifuatwa na Nairobi (51), Mashariki (49) na Pwani (48).

Tatizo la ukosefu wa ajira ni kubwa zaidi Nairobi kwa asilimia 39, Magharibi (31) na Mashariki (30).

Gharama ya juu ya maisha nayo imelemea zaidi wakazi wa Kati na Rift Valley kwa asilimia 25 kila moja, Mashariki (24) na Pwani (21).

Asilimia 55 ya Wakenya nao wanaamini kuwa Rais Kenyatta ndiye mwenye uwezo wa kubadilisha mkondo wa nchi kuwa mzuri, huku asilimia 17 wakisema ushirikiano wa Rais na Bw Odinga unaweza kusaidia kurekebisha hali ya nchi na asilimia saba wakisema ushirikiano wa Rais na Dkt Ruto unahitajika katika kuboresha mambo.

Wale ambao wanaamini nchi iko kwenye mkondo mzuri ni asilimia 34, ambao wanatoa sababu kuu kuwa ni amani inayoshuhudiwa nchini tangu handisheki, juhudi za kupiga vita ufisadi, umoja kati ya serikali na upinzani, uchumi kuimarika pamoja na jitihada za kupambana na wanaovunja sheria.

Mkoa wa Kaskazini Mashariki unaongoza kwa idadi ya wanaoamini mambo ni mazuri kwa asilimia 47 ya wakazi ukifuatwa na Nyanza na Rift Valley.

Utafiti huo hasa kuhusu matatizo yanayokumba wananchi wengi unadhihirisha manung’uniko ambayo yamekuwepo miongoni mwa wananchi wa kawaida wanaohisi Serikali ya Jubilee imeshindwa kushughulikia shida zao.

Ukosefu wa kazi hasa unahangaisha vijana wengi na idadi hii inaendelea kuongezeka, na wanasema Serikali imekosa kutimiza ahadi ilizowapa za kuweka sera mwafaka za kubuni nafasi za kazi.

Kwenye manifesto yake, Jubilee iliahidi kubuni nafasi za kazi 1.3 milioni kila mwaka.

Kulingana na takwimu za serikali, nafasi 897,000 za kazi zilibuniwa 2017 nyingi zikiwa katika sekta ya jua kali.

Ni nafasi 110,000 za kazi za watu waliosomea taaluma mbalimbali zilizobuniwa katika kipindi hiki.

Kuhusu siasa, Wakenya wengi wanaamini kuwa upinzani umeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa kushindwa kuhakikisha Serikali inatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Kulingana na matokeo ya utafiti huo, ni asilimia 25 ya watu waliosema upinzani unatekeleza wajibu wake.