Habari Mseto

Raia wa Iran wanaotuhumiwa kwa ugaidi waishtaki serikali ya Kenya

March 14th, 2018 1 min read

Raia wawili wa Iran Mabw Ahmad Abolfathi Mohammed na Sayed Mansour Mousavi wakiwa katika mahakama ya juu Machi 13. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wawili wa Iran waliozuiliwa baada ya kuachiliwa huru kwa kosa la ugaidi na mahakama ya rufaa Jumanne walimshtaki mwanasheria mkuu kwa kukaidi agizo la Mahakama ya Juu kwamba wazuiliwe katika mazingira mema.

Wawili hao wanadai kinyume na maagizo ya mahakama ya juu wazuiliwe katika mazingira ambapo haki zao hazikandamizwi, bado wanatesekea katika afisi za polisi wa kupambana na ugaidi ATPU.

Na wakati huo huo Serikali ilimteua wakili mwenye tajriba ya juu Bw Waweru Gatonye kuitetea Serikali katika kesi iliyowasilishwa na raia hao wa kigeni Mabw Ahmad Abolfathi Mohammed na Sayed Mansour Mousavi.

Mousavi na Abolfathi wanamsihi Jaji Mkuu aliye pia rais wa mahakama ya juu (CJ) David Maraga , Majaji Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala na Njoki Ndung’u wamchukulie hatua Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) kwa kukaidi haki zao.

Wawili hao wanasema tangu Feburuari 23 wamekuwa wakizuiliwa katika hali duni kinyume na agizo la mahakama kwamba haki zao zisikandamizwe kwa kuzuiliwa katika hali isiyoridhisha.

Kufuatia kuteuliwa kwa Bw Gatonye kuongoza kesi hiyo ambapo Serikali inapinga kuachiliwa kwa wawili hao mahakama ililazimika kuahirisha kesi impe fursa ya kujiandaa.

“Niliteuliwa  Jumatatu kuitetea Serikali katika kesi hii kisha nikakabidhiwa nakala nyingi za kesi hii na wakili Ahmednassir Abdullahi. Nahitaji muda wa kujiandaa ndipo niitetee serikali ipasavyo,” alisema Bw Gatonye.

Wakili huyo alisema kuna masuala mazito mno ya kisheria katika kesi hii na yanahitaji muda kung’amuliwa,” alisema Bw Gatonye.

Ombi hilo la kuahirishwa kwa kesi hiyo ilipingwa vikali na Bw Abdullahi akisema “uteuzi wa Bw Gatonye ni mbinu ya kuchelewesha kuamuliwa kwa kesi hiyo.”

Lakini Jaji Maraga alimkubalia Bw Gatonye ajiandae na kuamuru kesi isikizwe  kuanzia Machi 28, 2018.