Habari Mseto

Raia wa Rwanda apatikana na hatia ya kumuua mwanamke mjamzito lojing'i

October 18th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Alhamisi ilimpata raia wa Rwanda na hatia ya kumuua mwanamke mjamzito.

Jaji Jessie Lesiit alimpata na hatia Antoinette Uwineza almaarufu Micheline Uwababyi ya kuua akikusudia.

Jaji huyo alisema upande wa mashtaka ulithibitisha Antoinette alimuua mwenzake waliyekuwa wanang’ang’ania mwanamume mmoja raia wa Uingereza.

“Hii mahakama imekupata na hatia ya kuua. Utakaa rumande hadi Oktoba 23, 2018 utakaporudishwa tena kortini kujitetea kisha mahakama ikueleze utakachofanya,” alisema Jaji Lesiit.

Bi Uwineza aliondolewa mahakamani na kurudishwa gereza la wanawake la Lang’ata huku washtakiwa wawili waliokuwa wameshtakiwa pamoja Alexander Kiole Mutie na Kassim Oyamo Odiwuor almaarufu Odi wakiachiliwa.

Odin na Bw Mutie walihusishwa na mauaji hayo kwa kupatikana na simu ya marehemu.

Mutie alimweleza Jaji Lesiit aliuziwa simu hiyo na Odi aliyesema akijitetea kuwa aliinunua kutoka kwa jamaa.

Marehemu alikutwa ameuawa ndani ya lojing’i katika barabara ya River Road, Nairobi.

Alivishwa mfuko wa plastiki kichwani baada ya kunyongwa.