Habari Mseto

Raia wa Uganda kizimbani kwa kuwatapeli Wakenya mamilioni

October 16th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Uganda Jumanne alishtakiwa kwa kuwalaghai wafanyabiashara wa Kenya Sh12.3 milioni akidai atawawekezea katika wakfu ulioko nchini Uganda.

Bi Audrey Nabasaa alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama  ya Milimani Nairobi.

Alikanusha mashtaka ya kuwalaghai wanawake wanaofanya biashara jijini Nairobi viwango mbali mbali vya pesa.

Alishtakiwa mnamo Julai 20 mwaka huu akishirikiana na watu wengine wanaoendelea kusakwa na Polisi alipokea Dola za Marekani $30,000 (Sh3 milioni) kutoka kwa Bi Eunice Nyambura Chege akidai amwekezea pesa hizo katika kampuni ya Melchizedeck Investiment Group (MIG) yenye makao yake makuu nchini Uganda.

Mshtakiwa alikuw amewaeleza wawekezaji hao kwamba watakuwa wanapokea marupurupu kutoka kwa hazina kuu ya Herge iliyoko Uganda.

Wengine ambao Bi Nabasaa aliowafuja ni Bi Everlyne Muthoni Mutuku $21,500 (Sh2,150,000) ,  Bi Martha Wamaitha $22,500 (Sh2,225,000), Bi Catherine  Gathoni $22,500 (Sh2,250,000) , Bi Susan Njeri Ngandu $11,500 (Sh1,150,000), Bi Bilha Nyambura Chege $7,500(Sh750,000) na Bi Joyceline Wairimu Chege$750,000(Sh750,000).

Mahakama ilifahamishiwa kuwa mshtakiwa anakabiliwa na shtaka lingine sawa na hilo la ulaghai na ameachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.

Wakili anayemtetea mshtakiwa aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu kama vile Sh500,000 pesa tasilimu

Kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi alieleza mahakama kuwa kesi ya jana ni tofauti kabisa na kesi hiyo ya awali.

Mahakama ilimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh2 milioni na kuorodhesha kesi hiyo kusikizwa Novemba 22 mwaka huu.

Mshtakiwa alifahamishwa akishindwa kulipa pesa hizi awasilishe kortini dhamana ya Sh3milioni kisha athaminiwe na raia wa Kenya.