Habari Mseto

Raia wa Zimbabwe pabaya kwa kuiba mali ya Oilibya

October 11th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KINARA wa kampuni ya kuuza mafuta ya Oilibya amepata afueni mahakama kuu ilipomzuia mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji kuendelea na kesi  dhidi yake ya uvunjaji na wizi kutoka kituo cha kuuza mafuta kinachomilikiwa na wafanyabiashara wa humu nchini.

Bw Duncan Ziyanai Murashiki (pichani), raia wa Zimbabwe, ameshtakiwa pamoja na wafanyakazi wakuu wa Oilibya kwa wizi wa mali yenye thamani ya Sh1.5 milioni.

Mnamo Juni 2018 , Bw Haji aliamuru Bw Murashiki na Bi Joyce Nekoye Wanjala , Nancy Waeni Mutune Kwinga , Antony Muraya Mugo na Stanley Marete washtakiwe upya baada ya kutamatishwa kwa kesi hiyo hiyo Machi 15 2018.

Bw Haji aliamuru wakamatwe na kushtakiwa mara moja.

Sasa Murashiki na wenzake waliwasilisha kesi katika mahakama kuu wakipinga hatua hii ya Bw Haji wakisema haki zao zimekiukwa.

Watano hao pamoja na kampuni ya Oilibya walimweleza Jaji Pauline Nyamweya kuwa mzozo baina yao na wamiliki wa kampuni ya Maced unatokana na kuvunjwa kwa mkataba wa kibiashara.

Walimweleza jaji huyo kesi ya kusuluhishwa kwa mzozo huo wa kibiashara inaendelea na “hawapasi kushtakiwa kwa makossa ya uhalifu.”

Lakini Maced imeomba mahakama kuu isiwasikize washtakiwa hao kwa vile walitekeleza uhalifu kwa kuvunja kituo cha Petroli cha Juja Road Service Station na kuiba mali yenye thamani ya Sh1.5milioni.

Kesi hiyo itasikizwa Desemba 18.