Kimataifa

Raia waandamana kupinga Spika kuteuliwa Rais mpya Algeria

April 11th, 2019 2 min read

NA MASHIRIKA

MASENETA nchini Algeria Jumatano walimchagua Spika wa Bunge la Seneti Abdelkader Bensalah ambaye ni mshirika wa karibu wa kisiasa wa Rais wa zamani Abdelaziz Bouteflika kuwa Rais wa muda wa taifa hilo.

Kuteuliwa kwa Bw Bensalah hata hivyo kuliwakera waandamanaji ambao walihusika pakubwa katika kuhakikisha utawala wa zaidi ya miaka 20 wa Bw Bouteflika unafikia ukingoni mwezi uliopita.

Bw Bensalah alichaguliwa Rais mshikilizi kufuatia hitaji la katiba linalomtunuku wadhifa huo kwa kipindi cha siku 90 hadi uchaguzi mpya uandaliwe kisha Rais mpya achaguliwe.

“Ninataka kufanya kazi kwa njia ambayo itawaridhisha wananchi wa Algeria. Ni jukumu kubwa ambalo nimetwikwa na katiba ya nchi,” akasema Bw Bensalah mwenye umri wa miaka77, miaka mitatu tu chini ya ule wa Bw Bouteflika ambaye ana umri wa miaka 80.

Waandamanaji waliokuwa wanaendesha juhudi za kumaliza utawala wa Bw Bouteflika pia waliwataka washirika wake kama Rais Bensalah waondoke naye.

Kufuatia uteuzi wa Rais huyo mshikilizi, vyama vya upinzani jana vilijitokeza kukataa kumkubali na hata kutohudhuria hafla ya kukabidhiwa kwake mamlaka ndani ya seneti.

Mamia ya wanafunzi vile vile walikusanyika katika mji mkuu wa Algiers wakiandamana kuwasalisha ujumbe wa kupinga uteuzi wa mkongwe huyo na kumtaka ajiuzulu jinsi Bw Bouteflika alivyofanya. “jiuzulu, Bensalah’’ wakaimba wanafunzi hao waliobeba mabango na bendera za Algeria.

Kabla ya kikao cha jana bungeni, kulikuwa na makala ndefu kwenye jarida maarufu la serikali kwa jina El Moudjahid siku ya Jumanne iliyomrai Bw Bensalah kujiuzulu ili asikabadhiwe wadhifa wa Urais.

“Hakaribishwi katika wadhifa huo na wananchi, viongozi wa upinzani na makundi ya kisiasa. Pande zote hizi zimekuwa zikimshinikiza aondoke mara moja,” ikasema makala kwenye jarida hilo. Mnamo Ijumaa wiki jana wakati wa maandamano makubwa tangu Rais wa zamani aondoke madarakani, waandamanaji walisisitiza kwamba washirika wake waliokuwa wakishikilia nyadhifa zingine pia waondoke pamoja naye.

“Lazima ajiuzulu, ni sauti za wananchi inayozungumza na wananchi wako sawa. Hawajui kwamba kuna demokrasia na nataka kuwafundisha maana ya uhuru ,” akasema moja wa waandamanaji kwa jina Mourad, 50 ambaye ni mfanyabiashara.

Bw Mourad ameahidi kurejelea maandamano hayo wakati wa swala la Ijumaa kesho pamoja na bintiye wawili hadi Bw Bensalah asalimu amri.

Waandamanaji wameendelea kukiuka marufuku ya serikali kutoandamana huku Shirika la Kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch likitaka wakuu wa serikali kufutilia mbali marufuku hiyo.