Raia wachoka

Raia wachoka

Na MASHIRIKA

WIMBI la maandamano linaendelea kutanda ulimwenguni, mataifa ya Lebanon, Chile, Ecuador na Haiti yakiwa ya hivi punde kushuhudia hali hiyo.

Maandamano hayo yote yamesababishwa na malalamishi ya raia kuhusu kuporomoka kwa uchumi, mfumkobei hasa wa bidhaa muhimu na za kimsingi, ushuru wa juu na vitendo vya ufisadi miongoni mwa wanasiasa.

Maandamano Chile, Haiti, Lebanon kuhusu uchumi

Jumatatu, maelfu ya raia katika nchi za Lebanon, Chile na Haiti waliendelea na maandamano makubwa ya kupinga kunyanyaswa kiuchumi na vilevile kukithiri kwa visa vya ufisadi.

Maandamano hayo yanafuatia mengine katika nchi ya Ecuador ambayo yalilazimisha serikali kufuta utekelezaji wa nyongeza ya bei ya mafuta na sera zingine ambazo zingeongeza gharama ya maisha kwa raia.

Maandamano makubwa zaidi yalishuhudiwa Lebanon katika Mashariki ya Kati, ambapo raia kote nchini humo walijitokeza barabarani kupinga ushuru mpya na matatizo ya kiuchumi

Maandamano hayo yalianza wiki iliyopita katika jiji kuu Beirut baada ya serikali kupendekeza kuongeza ushuru kwa raia.

“Nimejitokeza kwa sababu nimekasirishwa na wanasiasa. Hakuna wanachofanya kusaidia raia,” akasema mmoja wa waandamanaji.

Raia pia wanataka kukomeshwa kwa ufisadi wakisema viongozi wamekuwa wakitumia mamlaka yao kujitajirisha kupitia kandarasi na kupokea hongo

Nchini Chile ambayo iko Amerika Kusini, raia walianza maandamano kupinga ongezeko la nauli pamoja dhuluma zingine za kiuchumi kutoka kwa serikali yao.

Licha ya Chile kuwa na mapato ya juu zaidi Amerika Kusini, kumekuwa na malalamiko kuhusu sera za kiuchumi ambazo zimesababisha gharama ya juu kwa huduma muhimu kama afya, elimu na vyakula.

Wiki iliyopita, serikali ya Ecuador ililazimika kubadilisha uamuzi wake wa awali wa kuongeza bei ya mafuta, ushuru na sera zingine ambazo raia walisema zinawanyanyasa.

Bei ya mafuta

Waandamanaji walianza maandamano Oktoba 3 baada ya Rais Lenin Moreno kuongeza bei ya dizeli maradufu na ya petroli kwa asilimia 30.

Serikali pia ilitangaza kupunguzwa kwa mishahara ya wafanyikazi wapya wa umma kwa asilimia 20, watumishi wa umma kuchangia serikali mshahara wa siku moja kila mtu kwa kila mwezi na kupunguzwa kwa muda wa likizo kutoka siku 30 hadi 15.

Maandamano hayo yalianzishwa na madereva wa teksi, trela na mabasi kwa kufunga barabara, hali iliyokwamisha shughuli kote nchini humo.

Raia wengine wakiongozwa na makundi ya wanafunzi, watetezi wa haki za binadamu, vyama vya wafanyikazi na vya uchukuzi walijiunga na maandamano hayo siku chache baadaye.

Maelfu ya raia wa Haiti nao jana waliandamana katika mji mkuu wa Port-au-Prince wakitaka Rais Jovenel Moise ajiuzulu kutokana na uzembe na utendakazi mbovu.

Uongozi wa Rais Moise ambaye aliingia mamlakani kwenye uchaguzi tata wa 2017 umekuwa ukikabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi huku pia upinzani ukikataa kutambua utawala wake.

You can share this post!

MSWAKI: Vikosi vya Uingereza kuwa na mteremko

Wakadiria hasara baada ya moto kuteketeza nyumba nne Likoni

adminleo