Raia waendeleza maandamano kupinga mapinduzi ya kijeshi

Raia waendeleza maandamano kupinga mapinduzi ya kijeshi

NA AFP

Naypyitaw

NAYPYITAW, Myanmar

MAELFU ya raia wa Myanmar jana Jumapili waliandamana kote nchini humo kupinga mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika wiki jana na kuwataka wanajeshi wamwachilie Rais Aung San Suu Kyi aliyeondolewa mamlakani.

Jana, maelfu ya raia waliovalia kofia na shati nyekundu pamoja na kubeba bendera nyekundu ambayo ni rangi ya chama cha NLD cha Suu Kyi, waliandamana na kushutumu jeshi kwa kuvuruga amani ya nchi hiyo kupitia udikteta.

“Hatutaki udikteta wa kijeshi, tunataka demokrasia,” wakaimba waandamanaji hao.

Wakuu wa jeshi wa Myanmar walitwaa madaraka kimabavu Jumatatu iliyopita na kuvuruga utawala wa mpito uliosifiwa ulimwenguni kwa kuhakikisha kuna demokrasia katika taifa hilo lililosambaratika kutokana na vita hapo awali.

Maandamano ya jana yalikuwa makubwa zaidi kuliko ya Jumamosi licha ya wakuu wa jeshi kuzima huduma za mtandao ili kulemaza maasi kutokana na hatua yao ya kumbandua kiongozi huyo madarakani.

Madereva walipiga honi, waandamanaji wakiiimba nyimbo za kumsifu Suu Kyi ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Hadhi ya Nobel.

“Hatutaki kuishi chini ya uongozi wa wanajeshi wenye utawala wa kimabavu,” akasema mwandamaji Ye Yint mwenye umri wa miaka 29.

Wakuu hao wa jeshi jana mchana, walirejesha huduma za mtandao suala ambalo lilikuwa limewakera waandamanaji na kuwakera zaidi kupigania Rais wao.

Halaiki ya waandamanaji waliotoka pembe zote za mji wa Yangon, walikusanyaka na kuelekea katikati mwa jiji la Pagoda ambalo lilikuwa kitovu cha maandamano makali ya miaka ya themanini na 2007.

“Hatutaki udikteta kwa kizazi cha sasa na kijacho. Hatutachoka kuandamana hadi tupate haki na Rais wetu awachiliwe. Tutapigana hadi mwisho,” akasema mwandamanaji mwengine, Thaw Zin, 21.

Inakadiriwa kwamba watu 1,000 walijiunga na maandamano hayo katika jiji la Naypyidaw na watu 60,000 kwenye mji wa Yangon pekee. Maandamano pia yaliripotiwa katika jiji kubwa la pili la Mandalay na mengine katika taifa hilo lenye watu milioni 53.

Ghasia hata hivyo zilishuhudiwa jiji la Myawaddy linalopatikana Kusini mwa Myanmar, kundi la waandamanaji lilipokabiliana na maafisa wa polisi.

Hata hivyo, hakuna visa vyovyote vya majeruhi vilivyoripotiwa.

Zaidi ya watu 160 wamekamatwa tangu jeshi litekeleze mapinduzi kulingana na Thomas Andrew ambaye ni mwanahabari wa Umoja wa Mataifa, Myanmar.

You can share this post!

Karua: BBI ni hujuma kwa Katiba

Gor, AFC Leopards waumiza nyasi bure alasiri nzima