Raia wafa njaa viongozi wakipiga domo

Raia wafa njaa viongozi wakipiga domo

Na WAANDISHI WETU

WAKENYA kadha katika Kaunti ya Samburu wamefariki kwa kukosa chakula na maji kufuatia ukame unaokumba kaunti 12 za eneo la Kaskazini Mashariki, Pwani na Mashariki mwa Kenya.

Huku viongozi wakizama kwenye siasa za urithi wa urais 2022, athari za ukame pia zimeshuhudiwa kaunti za Turkana na Baringo eneo la Rift Valley ambako wakazi wanakodolea macho kifo kwa kukosa chakula na maji.

Vijiji kadhaa katika eneo la kaskazini mashariki vimejaa harufu ya mizoga ya mifugo wanaofariki kwa kukosa lishe na maji sawa na wenyeji wanaopaswa kuwatunza.

Hali ni mbaya katika kijiji cha Kaliwalan, Samburu Kaskazini ambapo Angoomo Lokwaliwa, mwanamke mwenye umri wa miaka 35 na mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano, walifariki wakiwa kwenye safari ya kutafuta maji na chakula.

Wawili hao hawakuweza kupata chochote cha kula au kunywa kuweza kuokoa maisha yao.

Marehemu alikuwa kwenye kundi la watu waliokuwa wakitembea eneo la milimani la Baragoi kutafuta chakula na maji.

Kwa kulemewa na njaa, hakuweza kuendelea pamoja na mtoto wake aliyekuwa dhaifu kwa kukosa chakula mwa siku kadhaa.

Samuel Silale, msimamizi wa kijiji, alisema lilikuwa tukio la kutamausha.

“Kwa miaka ambayo nimeishi katika ulimwengu huu, sijaona kitu kibaya kama hiki,” Bw Silale aliambia Taifa Leo.

“Marehemu alikuwa katika kundi la watu waliokuwa wakienda Baragoi lakini akaachwa nyuma kwa kuwa alikuwa dhaifu. Hakuweza kutembea au kupiga nduru kuomba usaidizi. Wawili hao walipoteza maisha yao. Tuko katika hali mbaya,” alisema.

Anasema katika miezi kadhaa iliyopita, kiangazi kimezidi kuuma eneo hilo huku watoto na akina mama wakilazimika kutembea umbali wa kilomita 80 kutafuta matunda mwitu na maji.

Katika kijiji kilichohamwa cha Parikati, Antonella Arunye na wajukuu wake huwa wanalala njaa huku watoto hao sita wakiwa wameathiriwa na utapia mlo.

Huku mashavu yake yakiwa yamezama, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 54 anasimama karibu na manyatta yake akieleza masaibu anayopitia yeye na wajukuu wake.

“Huwa tunategemea maziwa ya mbuzi lakini wanyama wote wamekufa na waliobaki wamekonda. Tutaenda wapi? Hatujapokea msaada wowote. Sihitaji chochote isipokuwa chakula kwa watoto wangu ambao wanakabiliwa na hatari ya kufa kwa kukosa chakula,” alisema.

Hali ni sawa katika bonde la Suguta ambako Tioko Arikor anasema watu wengi wanaishi kwa kutegemea maji ya chumvi na matunda ya mwituni.

Watu wengi wanaishi kwa kutegemea maji ya chumvi na matunda wanayotembea mwendo mrefu kutafuta msituni.

“Tunalazimika kula matunda ya mwituni kuzima makali ya njaa ili tusifariki. Utapiamlo unaua watoto na wazee,” alisema.

Kulingana na idara ya mipango maalumu kaunti ya Samburu, zaidi ya watu 100,000 katika kaunti hiyo wanahitaji misaada ya chakula na maji.

Katika eneo la Tiaty, Baringo Kaskazini, wanawake na watoto wanalazimika kutafuna matunda hatari ya mwituni kuzima makali ya njaa.

Kaunti ambazo wakazi wako katika hatari ya kufa kwa sababu ya njaa ni Garissa, Wajir, Mandera, Isiolo, Samburu, Turkana, Marsabit. Baringo, Kilifi, Tana River, Kitui, Lamu, na Laikipia.

GEOFFREY ONDIEKI, MAUREEN ONGALA, KALUME KAZUNGU na FLORAH KOECH

You can share this post!

Uhuru, Raila wahudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais...

Wafanyabiashara walia ushuru ghali wamnyonga raia