Habari

Raia wengi wasio na hatia waangamia Libya, wanachama baraza la UN wakutana

July 4th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

TRIPOLI, LIBYA

BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya mkutano wa dharura Jumatano baada ya shambulio la bomu katika kituo cha kudhibiti wakimbizi na wahamiaji katika jiji kuu Tripoli lililosababisha vifo vya watu 44 na kuacha 130 wakiwa na majeraha.

Baraza hilo lenye wanachama 15 lilishindwa kuja na taarifa ya pamoja kama sehemu ya kujibu tukio hilo la shambulizi, katika kikao kilichofanyika faraghani.

Haya yanajiri huku kukiwa na taarifa kwamba idadi ya waliofariki kwenye msururu wa mashambulizi yakifikia idadi ya watu 55.

Serikali ya nchi hiyo yenye uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa imekashifu mpiganaji Khalifa Haftar aliyeagiza vikosi vitiifu kwake kuliteka jiji kuu mnamo Aprili.

Mjumbe wa UN nchini Libya, Ghassan Salame ametaja mashambulizi hayo kuwa “uhalifu wa kivita” kwa sababu yanawalenga watu wasiokuwa na hatia.

Katibu wa UN, Antonio Guterres, kupitia msemaji wake, alituma taarifa akisema amesikitishwa na kuitisha uchunguzi ufanywe.

Mapema Jumatano, msemaji wa kitengo cha kukabiliana na majanga ya dharura nchini Libya, Osama Ali, alisema watu si chini ya 35 waliuawa na wengine 73 kujeruhiwa.

Kituo hicho kilicho katika eneo la Tajouraa, huwa na idadi ya watu 600; na sehemu iliyoshambuliwa ilikuwa na wakimbizi wanaume 150 na wahamiaji kutoka mataifa kadhaa ya Afrika, kwa mujibu wa afisa wa uhamiaji, Mabrouk Abdel-Hafiz, anayefanya kazi na serikali.

Aprili 2019 Haftar aliagiza vikosi vyake vya Libyan National Army (LNA) kutwaa jiji la Tripoli kutoka mikoni mwa serikali inayoongozwa na Fayez Serraj.