HabariSiasa

Raila aachwa mpweke wenzake wakipata mamlaka

February 8th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

BAADA ya kugombea urais mara nne bila mafanikio, kiongozi wa ODM Raila Odinga amebaki kutazama marafiki wake wa karibu wakiendelea kushinda urais katika nchi zao.

Hii ni baada ya Rais Fellix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuingia kwenye orodha ya marafiki wakubwa wa Bw Odinga ambao kwa sasa ni marais katika nchi zao

Kulingana na mdadisi wa siasa Bw Thomas Maosa ambaye pia ni wakili, Bw Odinga amekuwa akijikosesha urais kwa sababu ya kuvunja miungano ya kisiasa na vyama kinyume na marafiki wake.

“Ukiangalia marafiki wake ambao ni marais, walivumilia katika vyama vyao vya kisiasa na hata miungano kwa miaka mingi. Hawakuhamahama vyama au kuvivunja kama ambavyo Bw Odinga hufanya, ambaye tangu 1992 ameongoza vyama vingi,” alisema.

Urafiki wake na baadhi ya marais hao ni wa muda mrefu na wanamheshimu sana kama mtetezi wa demokrasia barani Afrika.

Rais Tshisekedi ni rafiki wa miaka mingi wa Bw Odinga na alizindua kampeni yake ya kugombea urais katika hoteli ya Serena jijini Nairobi baada ya wawili hao kukutana mwaka jana, ambapo duru zilisema Bw Odinga ndiye aliyempa moyo na ushawishi wa kugombea urais nchini mwake.

Ni kutokana na urafiki wa wawili hao ambapo Rais Tshisekedi aliamua Kenya kuwa nchi yake ya pili kutembelea baada ya kuapishwa mwezi uliopita, na alipofika hapa nchini Jumatano alikutana kwanza na Bw Odinga hata kabla ya kuonana na Rais Uhuru Kenyatta.

Mwezi uliopita Bw Odinga almtembelea rafiki yake mwingine wa karibu Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania jijini Dar el Salaam kwa kile alichotaja kama kubadilishana mawazo.

Bw Odinga ni rafiki wa karibu wa Rais Magufuli tangu wakiwa mawaziri wa barabara katika nchi za Kenya na Tanzania mtawalia.

Mwanawe Fidel Castro Odinga alipoaga dunia mnamo 2015, Rais Magufuli, ambaye alikuwa waziri wa ujenzi nchini Tanzania wakati huo, alihudhuria mazishi kama rafiki wa familia ya Bw Odinga.

Bw Maosa anasema tofauti na Bw Odinga ambaye amebadilisha vyama vya kisiasa, Rais Magufuli amevumilia ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka mingi akipanda ngazi hatua baada ya nyingine hadi akateuliwa mgombeaji urais wa chama hicho.

Rafiki yake mwingine ni Rais Nana Akufo Addo wa Ghana ambaye aligombea urais wa nchi hiyo mara tatu kabla ya kushinda mnamo 2016. Bw Odinga alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa kwake kwa mwaliko rasmi wa Rais kisha akahudhuria dhifa katika makazi yake.

Urafiki wa wawili hao ulidhihirika pia wakati Bw Odinga alipopewa heshima za kirais na hata mlinzi rasmi wa rais alipohudhuria mazishi ya aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan mwaka jana.

Rafiki mwingine wa miaka mingi wa Bw Odinga ni Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini. Wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, upande wa serikali ulimkataa Ramaphosa kuwa mpatanishi kwa kile upande wa serikali ulichosema ni urafiki wake na Bw Odinga na hivyo ilihofiwa angependelea upande mmoja.

Rais mwingine mwandani wa Bw Odinga ni Allasane Ouattara wa Ivory Coast, ambaye kabla ya kuingia mamlakani alikuwa kiongozi wa upinzani.

Ghasia zilipokumba nchi hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa 2010, Muungano wa Afrika (AU) ulimtuma Bw Odinga kumpatanisha Rais Ouattara na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Laurent Gbagabo.

Kwenye ujumbe wa Twitter mnamo 2013, Bw Odinga alifichua kuwa Rais Outtara ni rafiki yake mkubwa: “Nilikutana na rafiki yangu mkubwa Rais Allasane Outtara wa Ivory Coast mjini Abidjan.”

“Siasa za Kenya zinaweza kuwa tofauti na za mataifa mengine, lakini Bw Odinga amekuwa akijiharibia nafasi kwa kuvunja vyama na miungano. Rafiki yake Magufuli alikaa CCM kwa muda mrefu kwa subira sawa na Ramaphosa katika ANC,” Wakili Maosa alieleza Taifa Leo.

Baada ya sheria kubadilishwa kuruhusu vyama vingi nchini mnamo 1992, Bw Odinga alijiunga na Ford ambacho kiligawanyika ndipo akahamia Ford Kenya kabla ya kubuni NDP hapo 1994.

Mnamo 2000 alianza kushirikiana na KANU kabla ya kuhama na kujiunga na LDP mnamo 2002 iliyoungana na NAK kubuni muungano wa Narc.

Aliondoka Narc mnamo 2005 na kuunda ODM ambacho 2013 kiliungana na Ford Kenya na Wiper kubuni Muungano wa Cord.

Aliacha Cord na kubuni Muungano wa NASA kwenye uchaguzi wa 2017 ukishirikisha ANC, Ford Kenya na Wiper. Mwaka jana aliwaacha washirika wake wa NASA na kutangaza kushirikiana na Rais Kenyatta, hatua ambayo ilimaliza muungano huo.